Breaking

MADA YA NNE: HARAKATI ZA KUDAI UHURU WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR

  DHANA YA UHURU NA HARAKATI ZA KUDAI UHURU

Uhuru ni hali ya mtu au nchi kuamua na kufanya mambo yake bila kuingiliwa na mtu au taifa lolote iwe kiuchumi, kisiasa, kijamii au kiutamaduni.

Katika muktadha huu;-

Uhuru ni hali ya nchi kujikomboa kutoka kwenye ukoloni wa mataifa ya kibepari.

Harakati za kudai uhuru

Ø  Harakati za kudai uhuru wa Tanganyika na Zanzibar ni mchakato au juhudi za watu wa nchi hizo kutafuta uhuru kutoka kwa serikali za kikoloni.

Ø  AU ni ni hatua zilizochukuliwa na wananchi wa Tanganyika na Zanzibar ili kufanikisha kupata uhuru wao kutoka kwenye utawala wa kikoloni.

v  Tanganyika ilitawaliwa na:-

i.        Wakoloni wa kijerumani kuanzia mwaka 1885 hadi 1918.

ii.      Wakoloni wa Uingereza kuanzia mwaka 1919 hadi ilipopata uhuru mnamo mwaka 1961.

v  Zanzibar ilitawaliwa na:-

i.        Utawala wa kisultani kutoka oman kuanzia mwaka 1840 hadi 1890,

ii.       Utawala wa Waingereza kuanzia mwaka 1890 hadi 1963.

 

MISINGI YA KUDAI UHURU WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR

Ø  Watanzania walianzisha harakati za kudai uhuru baada ya kuanzishwa kwa serikali za kikoloni.

Ø  Sababu zilizosababisha watanzania kudai uhuru wao ni kama ifuatavyo:

 

a)      Unyonyaji wa mali na rasilimali:

Mfumo wa kikoloni ulikuwa wa kiunyanyasaji na kinyonyaji. Watanzania walinyonywa katika nchi yao.

Ø  Mathalani walifanya kazi katika maeneo mbalimbali kama vile mashambani , migodini n.k bila kupata ujira unaostahili.

Ø  Vile vile waliamuliwa kulima mazao yaliyoletwa na wakoloni kwa ajiri ya viwanda vyao.

Ø  Hali hii ilijenga msingi mmojawapo katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika na Zanzibar

b)     Sera za kibaguzi:

Sera mbalimbali za kibaguzi zilianzishwa kupitia huduma za jamii, kwa mfano wananchi walibaguliwa katika kupata huduma za jamii kama vile afya, elimu na makazi.

Ø  Wazungu, Waarabu na Waasia walipewa huduma bora wakati Waafrika wakipewa huduma duni au kutopewa kabisa.

c)      Ukandamizwaji wa waafrika:

Wakoloni walipofika walianza kupora ardhi nzuri ya uzalishaji mali kutoka kwa wenyeji.

Ø  Hivyo iliwalazimu wenyeji hao kufanya kazi katika mashamba ya kikoloni ili waishi, na walilipwa ujira kidogo au amna kabisa.

Ø  Pia wananchi walitozwa kodi kwa nguvu. Lakini pia walilazimishwa kujenga miundombinu mbalimbali mfano reli kwa nguvu

d)     Kudhihakiwa kwa mila na desturi za watanzania:

Wakoloni kupitia wamisionari walipiga marufuku mila za kiafrika.  Kwa mfano majina pamoja na dini za kiafrika zilionekana ni za kishenzi,

Ø  Pia baadhi ya vyakula, nguo, lugha na sanaa vilipigwa marufuku.

e)      Kuongozwa na wakoloni:

Wakoloni walitaka kutawala Tanganyika na Zanzibar kwa muda mrefu, hivyo mifumo ya kiutawala haikutoa nafasi kwa waafrika kuendelea na utamaduni wao wa kuongozwa na viongozi wao wa jadi. Hali hii iliondoa uhuru wa watanzania.

Ø  Hata pale viongozi wa jadi walipokuwa wakitawala kupitia mfumo wa uwakala, uamuzi wotw ulitolewa na wakoloni kupitia gavana, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya.

Ø  Hali hii iliwakasirisha Watanganyika na kuamua kuanzisha harakati za kudai uhuru.

 

MBINU ZILIZOTUMIKA KUDAI UHURU WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR

Ø  Harakati za kudai uhuru waTanganyika na Zanzibar zilitumia mbinu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuanzisha jumuiya, vyama na taasisi za kijamii za waafrika.

Ø  Malengo ya kuanzishwa kwa jumuiya, vyama na taasisi hizo yalikuwa ni kutetea na kudai haki za wafanyakazi, wakulima na wafanyabiashara.

Ø  Kadri muda ubavyoendelea, jumuiya vyama na taasisi hizo zilijihusisha na siasa na kuchangia sana katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika na Zanzibar

A: VYAMA VYA USHIRIKA NA WAKULIMA

Chama cha ushirika ni muungano wa watu waliokubaliana kuendesha shughuli zao za kiuchumi kwa pamoja ili kuinua hali zao za maisha.

Ø  Shughuli hizi ni kama vile kutafuta mahitaji yao ya chakula, elimu, uuzaji wa mazao yao na shughuli nyingine za uchumi zinazoweza kuendeshwa kwapamoja.

Ø  Vyama vya wakulima vilianzishwa na wakulima wenyewe katika maeneo ambapo mazao ya kibiashara yalilimwa.

Malengo ya vyama vya wakulima ni ;-

                                i.            Kudai bei nzuri ya mazao yao ,

                              ii.            Kupata masoko ya uhakika,

                            iii.            Kudai pembejeo na zana za kilimo,

                            iv.            Kupinga unyonyaji na kutozwa kodi kubwa ya mazao yao.

Mifano ya vyama vya wakulima ni Bukoba Buhaya Union(1924), Kilimanjaro native Planters Association (1925), Sukuma union (1930), Pare union (1949)

Ø  Kwa upande wa Zanzibar, kulikuwa na jumuiya mbalimbali zilizoundwa na makundi ya wakulima kwa malengo kama ya wenzao Tanganyika.

Ø  Vyama hivi vilitoa watu mbalimbali ambao walikuja kuwa viongozi wa kisiasa, kama Paul Bomani na Clement George Kahama.

Ø  Vilevile vyama hivi vilipinga uamuzi wa serikali ya kikoloni ambao ulikuwa unawakandamiza watanganyika na wazanzibar.

Ø  Vyama hivi pia vilitoa pesa kwa TANU, kuunganisha na kuhamasisha watu katika harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika.

 

B: VYAMA VYA WAFANYAKAZI

Ø  Waafrika waliokuwa wameajiriwa katika viwanda, mashamba, bandari na sehemu nyingine walianzisha vyama vyao vya wafanyakazi kwa lengo la kulinda na kutetea masilahi yao ya kikazi.

Ø  Mfano wa vyama vya wafanyakazi ni;-

·         Tanganyika Territory Civil Servants’ Association(TTCSA), kilichoanzishwa na Martin Kayamba mwaka 1922 huko Tanga, ambapo mwaka 1924 kilifungua tawi lake mjini Dar es Salaam.

·         Dock Worker’s Union(1937)

·         Railway African Civil Service Union(1920)

·         Tanganyika Federation of Labour (1955) chini ya uongozi wa Rashid Mfaume Kawawa.

Ø  Kwa upande wa Zanzibar kulikuwa na;-

·         Jumuiya ya mabaharia kwa ajiri ya kupigania haki za wafanyakazi katika vyombo vya baharini. Jumuiya hii iliundwa na Sheikh Abeid Amani Karume Mwaka 1939.

·         Federation of Zanzibar and Pemba Trade Unions (ZPFL) 1956.

Ø  Pamoja na juhudi zao za kutetea masilahi ya wafanyakazi, waliendelea kujadili masuala ya kisiasa na hatimaye walijihusisha na harakati za kudai uhuru

 

C: VYAMA VYA WAFANYABIASHARA

Vyama vya wafanyabiashara wa Kiafrika vilianzishwa nchini Tanganyika ili kuyalinda na kuyatetea masilahi ya wafanyabiashara wa kiafrika dhidi ya wafanyabiashara wa kigeni

Ø  Baadhi ya madai yao ilikuwa ni kupinga unyanyasaji katika masoko, kupinga kutozwa kodi kubwa n.k

Ø  Mfano wa vyama hivi ni African Commercial Association kilichoanzishwa mwaka 1934 chini ya Erica Fiah.

Ø  Kwa upande wa Zanzibar, kulikuwa na Jumuiya ya Wahindi iliyoundwa mwaka 1910.

Ø  Vyama vya kijamii viliendelea kukua mwaka hadi mwaka nchini Tanganyika na Zanzibar. Mfano wa vyama hivi ni Tanganyika African Association (TAA) kilichoanzishwa Dar es salaam mwaka 1929. Chama cha TAA kiliundwa na watumishi wa serikali na baadaye kikazaa chama cha siasa kiitwacho TANU.

Ø  Zanzibar kulikuwa na African Association na Shirazi Association. Jumuiya hizi ziliungana na kuunda Chama cha Ukombozi cha Afro-Shirazi Party (ASP) ambacho pia ndicho kiliungana na TANU kuunda chama cha mapinduzi (CCM) mwaka 1977

Ø  Pamoja na kutetea haki na masilahi ya wafanyabiashara, vyama hivi vilikuja kushiriki katika harakati za kudai uhuru, ikiwa ni pamoja na baadhi yao kubadilika na kuwa vyama vya siasa

 

D: VIKUNDI NA VYAMA VYA KIDINI

Dini za kikristo na kiislamu zilitumika kama vyombo vya kuwaunganisha watu na kuendeleza harakati za kudai uhuru Tanganyika na Zanzibar.

Miongoni mwa vikundi na vyama vya kidini vilivoanzishwa nchini Tanganyika ni;-

·         Al- Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika (1933),

·         The Watch Tower Church,

·         The African National Church

·         The Church of God

Ø  Vikundi hivi vilitoa viongozi shupavu kama Ally Sykes, Bibi Titi Mohamed, Tewa Said Tewa na wazalendo wengine ambao walishirikiana na mwalimu JK Nyerere katika mapambano ya kudai uhuru wa Tanganyika

E: VILABU VYA MPIRA WA MIGUU

Vilabu vya mpira wa miguu vya Waafrika vilianzishwa na kusaidia kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa Waafrika sambamba na kueneza fikra za ukombozi dhidi ya madhila ya wakoloni.

·         Zanzibar mwaka 1931 ilianzishwa  klabu ya mpira wa miguu ,The African sport club ambayo kiongozi wake alikuwa sheikh Abeid Amani Karume .

·         Kwa upande wa Tanganyika, mwaka 1935 ilianzishwa klabu ya waafrika yenye jina la Young African Sport Club

Ø  Vilabu hivi vilihamashisha waafrika kujiunga na vyama pamoja na jumuiya kama vile TAA. Pia vilitoa michango mkubwa wa kuchangisha fedha kwa wanachama wao pamoja na kuwahamasisha kujiunga na vyama vya TANU na ASP

 

F: VYOMBO VYA HABARI

Kuanzishwa kwa vyombo vya habari Tanganyika na Zanzibar kuliongeza na kuimarisha harakati za waafrika katika kupigania uhuru wao.

Ø  Kwa upande wa Tanganyika, mfano wa vyombo hivyo ni;-

·         Gazeti la kwetu, lililoanzishwa na jumuia ya African Association (AA) mwaka 1937.

·         Sauti ya TANU, ambalo lilihaririwa na Mwalimu J.K Nyerere mwaka 1957.

Ø  Kwa upande wa Zanzibar kulikuwa na, kwa mfano,

·         Gazeti la Sauti ya Zanzibar (1949)

·         Gazeti la samachar lililoandikwa na Bwana Mtoro bin Abu Rehan

·         Magazeti mengine ni Afrika kwetu, mwongonzo, jasho letu, mkombozi, mwiba, sauti ya afro-shirazi, sauti ya jogoo na umma

Ø  Vyombo vya habari vya Waafrika vililenga kuamsha ari ya uzalendo kwa Watanganyika na Wazanzibar ili kuwaunganisha katika kudai uhuru wao.

Ø  Aidha vilitumika kupaza sauti dhidi ya maovu yaliyokuwa yakifanywa na serikali ya kikoloni

 

G: VIKUNDI NA VYAMA VYA SANAA

Wakati wa utawala wa kikoloni hakukuwa na nafasi ya kutosha kwa Watanganyika na Wazanzibari kusimamia na kujieleza kwa uhuru kuhusu haki zao na harakati za ukombozi.

Ø  Badala yake, mambo mengi ya harakati za kudai uhuru yalifanyika kwa siri kuhofia adhabu kutoka kwa wakoloni.

Ø  Viongozi na wanachama wa TANU na ASP waliamua kutumia sanaa na michezo kama mbinu mbadala.

Ø  Sanaa ilitumika katika kukuza na kuendeleza harakati za kudai uhuru wa Tanganyika na Zanzibar. Walianzisha vikundi na vyama vya sanaa na michezo kama vile kikundi cha taarabu cha Jipisheni (Egyptian Music Club) na Al-Watan

Ø  Vikundi hivyo vilikuwa vinafanya matamasha na mwalimu Nyerere alialikwa kama mgeni rasmi. Mwalimu nyerere alisimama kufungua hafla hizo na kwa kufanya hivyo, alisema maneno machache kuhusu harakati za kudai uhuru

Ø  Vilevile kupitia taarabu, TANU ilikusanya fedha kwa ajili ya kuendeleza harakati za ukombozi

 

H: VYAMA VYA SIASA

v  Umoja wa Waafrika ulioitwa African Association (AA) uliundwa mwaka 1929 na mnamo mwaka 1948 ulipewa jina jipya la Tanganyika African Association (TAA).

Ø  Mwaka 1954, chama hiki kilibadilishwa jina tena na kuwa chama rasmi cha siasa kwa jina la TANU.

Ø  TANU ilikuwa na malengo mbalimbali kama vile;-

i.        Kuwaunganisha wananchi wa Tanganyika na kuwaongoza katika mapambano ya kupigania uhuru wa nchi yao,

ii.      Kutoa tafsiri mpya ya ukombozi pamoja

iii.    Kuweka juhudi na fikra mpya za mapambano kwa msingi wa kifalsafa

iv.    kudai haki ya kuwa na wawakilishi wa kidemokrasia katika vyombo vya kutunga sharia

Ø  Vyama vingine ni  kama vile;-

i.        United Tanganyika Party (UTP) kilichoanzishwa mwaka 1956. Chama hiki kiliungwa mkono na wazungu, waasia na baadhi ya waafrika, hasa machifu.

ii.      African National Congress (ANC) kilichojitenga kutoka TANU mwaka 1958 na kuongozwa na Zuberi Mtemvu.

iii.    All Muslim National Union of Tanganyika (AMNUT). Chama hiki kilidai uhuru lakini walitaka mabadiliko ya katiba na uhuru viletwe polepole na si haraka kama TANU ilivyotaka.

Ø  Mpaka wakati wa uhuru, Tanganyika ilikuwa na vyama hivi vine

 

v  Kwa upande wa Zanzibar, vyama vilivyojitokeza kudai uhuru ni pamoja na

i.        Zanzibar Nationalist Party (ZNP) kilichoanzishwa kwaka 1955,

ii.      Afro-shirazi Party (ASP) Kilichoanzishwa mwaka 1959.

Ø  Vyama vyote hivi vilikuwa na lengo kuu la kudai uhuru wao.

Ø  Chama cha ASP kilikuwa na malengo ya

i.        kupigania uhuru wa Zanzibar,

ii.      kuunda serikali ya kidemokrasia katika visiwa vya unguja na pemba,

iii.    kuondoa ubaguzi wa aina yoyote katika visiwa hivyo,

iv.    kudumisha uhuru wa Zanzibar na watu wake

v.      kuwaandaa wananchi wawe tayari kupigania uhuru wao.

 

Mchango wa TANU na ASP katika harakati za kudai uhuru Tanzania.

i.        Vyama vya TANU na ASP viliunganisha wananchi na kuwaongoza katika mapambano ya kudai uhuru.

ii.      Vilihamasisha wananchi kujiunga navyo na kushiriki katika harakati za kuudai uhuru wan chi zao.

iii.    Vyama hivi viliandaa mikutano ya kisiasa na kuhamasisha wanachama pamoja na wanachi kuhudhuria mikutano hiyo.

iv.    Vilitoa elimu na mafunzo ya kiuongozi na kisiasa kwa viongozi wa matawi na kitaifa.

v.      Vyama vya TANU na ASP vilianzisha vyombo vya habari ili kuendeleza harakati za kudai uhuru.

 

MCHANGO WA HARAKATI ZA KUPINGA UVAMIZI NA UKOLONI

Mchango wa harakati za kupinga uvamizi wa kikoloni ulikuwa ni pamoja na kutunza maadili na kujenga uzalendo

1.      KUTUNZA MAADILI

Ø  Ujenzi wa maadili ni mchakato wa kihistoria kwa kuwa unatokana na hisia ambazo watu au jamii wamezikuza kwa miaka mingi kama sehemu ya harakati zao za kuleta maendeleo na uhuru katika jamii au nchi yao.

Ø  Maadili ni muhimu kutunza kwa vile yanaleta fahari, umoja, ujasiri, na mienendo inayokubalika katika jamii.

Ø  Hivyo, harakati za kupinga ukoloni nazo zilichangia katika utunzaji wa utambulisho wa mtanzania, ambao ni pamoja na utu, mshikamano na lugha ya Kiswahili.

 

A.    Kudumisha umoja

Harakati za kudai uhuru zilichangia pia kudumisha umoja.

Ø  Kabla ya uhuru, jamii za kitanzania zilikuwa zimegawanyika katika makabila mbalimbali. Kila kabila lilikuwa na utaratibu wake wa maisha ikiwemo mila na desturi zake.

Ø  Viongozi wa vyama vya TANU na ASP waliunganisha makabila na jamii mbalimbali.

Ø  Hali hii ilisaidia kudumisha maadili ya umoja kwani waliamini kuwa Umoja ni nguvu, Utengano ni udhaifu.

 

B.     Kutunza na kudumisha maadili ya Utu.

Ukoloni na mifumo yake iliathiri sana utu wa waafrika na hivyo kuamsha ari ya kupata uhuru ili kutunza maadili ya utu yaliyokuwa yamejengwa na jamii za asili za Tanganyika na Zanzibar.

Ø  Kwa hiyo, harakati za kupinga ukoloni pia zilichangia katika utunzaji na udumishaji wa maadili ya utu, kwani watanzania hawakuwa tayari kuona utu wao au maadili yao yakipotea

 

C.    Kudumisha mshikamano

Wakati wa kupinga uvamizi wa kikoloni, viongozi waliunganisha watu katika jamii zao ili kuwa na nguvu za kupambana na uvamizi wa kikoloni.

Ø  Viongozi kama vile Mtwa Mkwawa wa wahehe, Mangi Meli wa Old moshi, Mtemi Isike wa Unyanyembe na viongozi wengine walihamasisha watu wao kushikamana ili kukabiliana na uvamizi wa wakoloni wa kijerumani

Ø  Aidha, wakati wa harakati za kudai uhuru wa Tanganyika na Zanzibar, viongozi walihimiza mshikamano wa watanzania wote ili kuwawezesha Tanganyika na Zanzibar kupata uhuru

 

D.    Kukuza na kudumisha Kiswahili

Harakati za kupinga ukoloni na kupigania uhuru wa Tanganyika na Zanzibar zilitumia lugha ya Kiswahili kwa namna mbalimbali.

Ø  Mathalani, Kiswahili kilitumika kusaidia kuleta umoja na mshikamano miongoni wa wanachama wa TANU na ASP pamoja na wananchi wote.

Ø  Lugha ya Kiswahili iliwaunganisha wananchi wa jamii tofauti tofauti haijalishi makabila yao. Nyimbo, taarabu zilizokuwa zinatumiwa katika mapambano dhidi ya wakoloni zilikuwa katika lugha ya Kiswahili.

Ø  Vyombo vya habari kama magazeti mbalimbali yalitumia lugha ya Kiswahili katika kuelimisha na kutoa habari kwa wananchi kuhusu harakati za kupigania uhuru.

Ø  Sera na itikadi za TANU na ASP zilielezwa kwa lugha rahisi ya Kiswahili, hivyo kurahisisha ufikishaji wa ujumbe kwa wananchi.

Hivyo kupitia harakati za kudai uhuru, Kiswahili kilijiimarisha na kuenea zaidi nchini.

2.      KUJENGA UZALENDO

Harakati za kupinga ukoloni vilihusisha upiganaji wa vita dhidi ya wakoloni.

Ø  Katika harakati hizi, watanzania walionesha uzalendo kwa jamii zao pale waliposimama kidete kuupinga uvamizi na utawala wa kikoloni kwa sera zao za unyonyaji na ukandamizaji.

Ø  Baadhi ya watanzania waliochangia katika ujenzi wa uzalendo kwa jamii zao ni pamoja na Abushiri bin Salim al-Harthi wa Pangani, Mangi Meli wa Old Moshi, Mtemi Isike wa unyanyembe, Mtwa Mkwawa wa Iringa, Mwene Machemba wa Wayao, Nkosi Songea, Mbano wa Wangoni na Liti Kidanka wa Singida

Ø  Hivyo, harakati za wazalendo hawa kupinga uvamizi wa kikoloni, ulichangia katika ujenzi wa maadili ya uzalendo kwani wananchi walijitoa kushiriki katika vita na ulinzi wa jamii zao.

Ø  Harakati za kupinga ukoloni zilipanda mbegu ya uzalendo kwa jamii za kitanzania, kupenda jamii zao na hata kujitoa maisha yao kupambana dhidi ya uvamizi wa kikoloni. Hali hii ilichangia katika ujenzi wa kizalendo ndani ya jamii zao na baadaye kwa nchi nzima za Tanzania

Ø  Aidha, viongozi vya vyama vya TANU na ASP pamoja na viongozi wengine katika ngazi mbalimbali walikuwa wazalendo, kwani, walitoa mchango muhimu katika kuanzisha na kuendeleza harakati za kudai uhuru. Uzalendo wao ulidhihirika kupitia ushiriki wao katika kuanzisha na kusimamia vyama vya siasa.

 

ZOEZI

1.      Je, unafikiri ni kwa nini harakati za kudai uhuru wa Tanganyika na Zanzibar zilifanikiwa kuwaunganisha wananchi?

2.      Kwanini vyama vya TANU na ASP vilipata uungwaji mkono mkubwa ukivilinganisha na vyama vingine vya siasa wakati wa kupigania uhuru?

3.      Eleza kwanini uhuru wa Tanganyika na Zanzibar unapaswa kulindwa

4.      Fafanua maadili yaliyodumishwa wakati wa harakati za kudai uhuru wa Tanganyika na Zanzibar

5.      Kwa kutumia mifano, eleza maana ya uzalendo

6.      Jadili mchango wa viongozi wa kisiasa wa sasa katika kutunza maadili na kujenga uzalendo

7.      Eleza mchango wa mwalimu Julius Kambarage Nyerere na sheikh Abeid Amani Karume katika kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika na Zanzibar


MADA YA KWANZA:UKOLONI KATIKA JAMII ZA KITANZANIA

MADA YA PILI:UKOLONI KATIKA JAMII ZA KITANZANIA

MADA YA TATU: MAPAMBANO YA AWALI DHIDI YA UVAMIZI WA KIKOLONI

MADA YA NNE: HARAKATI ZA KUDAI UHURU WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR

MADA YA TANO: UJENZI WA TAIFA BAADA YA UKOLONI

MADA YA SITA: MAPINDUZI MATUKUFU YA ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment