Breaking

MADA YA KWANZA : UKOLONI KATIKA JAMII ZA KITANZANIA

CHIMBUKO NA UKUAJI WA UKOLONI

UKOLONI: Hii ni hali ya nchi moja kuitawala nchi nyingine katika Nyanja zote za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.

Ø  Katika muktadha huu, uchumi, siasa na utamaduni wa nchi zilizotawaliwa hutumiwa kwa malengo ya wakoloni.

Ø  Ukoloni ulitokana na kustawi kwa mfumo wa ubepari, ambao ulifikia hatua ya ubeberu huko ulaya magharibi.

Ø  Ubeberu huu uliwalazimu wakoloni kuvuka mipaka ya nchi zao ili kutafuta rasilimali na masoko mapya ya bidhaa zao na sehemu za kuwekeza mitaji.

Ø  Ukuaji wa ubepari katika robo ya karne ya 19 uliambatana na mapinduzi na maendeleo ya viwanda katika nchi za ulaya magharibi iliyosababisha ongezeko la mahitaji ya malighafi hasa za kilimo na madini. Malighafi kutoka bara la asia pamoja na kanada hazikutosheleza mahitaji ya viwanda.

 

SABABU ZILIZOWALAZIMU WAKOLONI KUVUKA MIPAKA YA NCHI ZAO NA KUINGIA BARA LA AFRIKA

i.                    Mahitaji ya malighafi

Ø  Maendeleo ya viwanda katika nchi za ulaya magharibi yalisababisha ongezeko la mahitaji ya malighafi hasa za kilimo (mf. Kahawa, katani, pamba n.k) na madini, kwaajili ya uzalishaji wa bidhaa viwandani. Malighafi kutoka bara la asia pamoja na kanada hazikutosheleza mahitaji ya viwanda.

Ø  Hivyo, mataifa kama uingereza, ufaransa, ujerumani, ubelgiji na ureno yalivutiwa na rasilimali hizo barani Afrika na kuamua kuzifuata ili kukidhi mahitaji ya viwandani.

ii.                  Mahitaji ya masoko

Ø  Mataifa ya ulaya yalihitaji masoko mapya ya bidhaa zilizozalishwa na viwanda vyao kama vile nguo, vioo, heleni, bangiri n.k. Hivyo makoloni ya Afrika yalionekana ni masoko mapya ya bidhaa zao za viwandani.

iii.                Mahitaji ya maeneo ya kuwekeza

Mataifa ya ulaya yalihitaji maeneo ya kuwekeza mitaji yao ili kupata faida kubwa. Hivyo bara la afrika lilionekana kuwa suluhisho kubwa kwa uwekezaji huo wa kibiashara.

iv.                Matamanio ya kueneza dini ya kikristo.

Ø  Wamisionari waliona ni wajibu wao kueneza maadili ya kikristo katika maeneo mbalimbali, hasa barani afrika. Wamisionari wa kwanza wa madhehebu ya kikristo katika jamii za kitanzania walikuwa Ludwig Krapf na Johan Rebman.

Ø  Wamisionari hawa walijifunza mila, desturi, maadili na mazingira ya kitanzania. Walijifunza pia fikra za wananchi na viongozi wa jadi, ili kujua namna ya  kuzitawala jamii hizo

v.                  Ushindani wa kisiasa na kijeshi.

Ø  Ushindani huu ulikuwa ndani ya mataifa ya ulaya magharibi kutawala maeneo makubwa. Lengo lilikuwa ni kudhihirisha nguvu zao za kiuchumi na kijeshi hasa kutawala maeneo muhimu ya kimkakati.

Ø  Sehemu hizo ni kama vile njia ya bahari ya shamu hadi bahari ya Hindi na mabonde muhimu kama vile  Kongo, Niger, Naili na Zambezi.

 

HIVYO, kutokana na sababu hizo, nchi za ulaya zilituma wapelelezi mnamo mwaka 1850 hadi 1870, na kugundua kuwa bara la afrika lina uwezo wa kuzalisha malighafi za kutosha kwa ajili ya viwanda vya ulaya magharibi, maeneo ya kutosha kwaajili ya uwekezaji na masoko ya didhaa za viwandani. Ukoloni ulishamiri barani afrika katika karne ya 19 na 20.

 

MBINU ZILIZOTUMIWA NA WAKOLONI KUANZISHA NA KUIMARISHA TAWALA ZAO

Wakoloni walitumia walitumia mbinu mbalimbali kuanzisha na kuimarisha tawala zao. Mbinu hizo ni pamoja na

        i.            Kusaini mikataba ya kilaghai.

Ø  Mikataba hiyo ilisainiwa kati ya viongozi wa jadi na mawakala wa kikoloni. Mikataba hiyo ilikuwa na masharti magumu na iliwanyima wenyeji (waafrika) haki ya kuhoji kabla ya kusaini.

Ø  Mfano ni mkataba uliosainiwa na Chifu Mangungo wa Usagara na Karl Peters, mwakilishi wa wajerumani mwaka 1885.

      ii.            Mbinu ya kuungana na baadhi ya jamii za kitanzania dhidi ya jamii zingine.

Ø  Hii ilitokea katika maeneo yenye uhasama mkali kati ya jamii za kitanzania. Mfano wajerumani waliungana na chifu Merere wa wasangu na baadhi ya viongozi wa wabena kuwapiga wahehe waliokuwa chini ya utawala wa Mtwa Mkwawa.

Ø  Vilevile, wajerumani waliungana na Mangi Mandara wa moshi kumpiga Mangi Sina wa kibosho.

Ø  Mara nyingi wakoloni waliungana na jamii dhaifu ili kuzipiga jamii zenye nguvu na hivyo lujipenyeza na hatimaye kuimarisha tawala zao.

    iii.            Kwa kutmia nguvu za kijeshi.

Ø  Njia hii ya matumizi ya nguvu za kijeshi (kivita) ilitumiwa zaidi kwani jamii nyingi za kitanzania hazikuwa tayari kuupoteza uhuru wao kirahisi.

Ø  Maeneo ambayo wenyeji walipinga uvamizi, walishindwa kutokana na sabau mbalimbali ikiwemo ubora wa silaha za kikoloni ukilinganisha na silaha za jadi zilizotumiwa na jamii ya kitanzania.

    iv.            Mkutano wa Berlin wa mwaka 1884-1885.

Ø  Mkutano huu ulilenga kuligawa Bara la Afrika miongoni mwa mataifa ya Ulaya. Hii ilileta madhara makubwa kwa jamii za kiafrika zilizokuwa zimejengwa kwa misingi ya utu, umoja, uzalendo na amani.

 

MIFUMO YA KIKOLONI YA MATAIFA YALIYOZITAWALA JAMII ZA KITANZANIA

Mifumo ya utawala ya waarabu, wajerumani na waingereza katika jamii za kitanzania ilitofautiana kwa kiasi kikubwa, ingawa lengo kuu la mifumo hiyo ilikuwa kunyonya na kupora rasilimali watu na rasilimali asilia za jamii za kitanzania

i.                    Waarabu wa mwanzo waliofika pwani ya afrika mashariki kabla ya karne ya 18, hawakuja kama wakoloni bali kama wafanyabiashara.

·         Hata hivyo, waarabu kupitia utawala wa sultani wa Zanzibar kuanzia karne ya 18, walijikita zaidi katika biashara, hususani biashara ya pembe za ndovu, watumwa, karafuu, na nazi.

·         Mfumo huu wa utawala ulitengeneza tabaka la juu la waarabu na wahindi na tabaka la chini la waafrika ambao walibaki katika hali duni kimaisha.

ii.                  Wajerumani walitawala jamii za kitanzania kuanzia mwaka 1885 hadi 1919 baada ya vita kuu ya kwanza ya dunia.

·         Wajerumani walitumia mfumo wa utawala wa moja kwa moja, uliokuwa na matumizi ya nguvu za kijeshi na sheria kali dhidi ya watawaliwa.

·         Mfano, Jamii za kitanzania ziliporwa ardhi kwa nguvu na kulazimishwa kufanya kazi katika mashamba na miradi ya kikoloni kama vile ujenzi wa reli.

iii.                Waingereza walitawala Tanganyika kuanzia mwaka 1919 baada ya vita kuu ya kwanza ya dunia hadi 1961.

·         Kuanzia mwaka 1919 hadi 1925, waingereza waliendeleza muundo wa utawala waliourithi kutoka kwa wajerumani.

·         Kuanzia mwaka 1926, chini ya uongozi wa Gavana Sir Donard Cameron, waingereza walibadilisha mfumo huo na kuanzisha utawala wa kiuwakala.

·         Katika mfumo huu mpya, walitumia mamlaka za jadi kutekeleza sera za kikoloni. Tofauti na utawala wa wajerumani, mfumo huu haukuwa na ukatili mkubwa.

 

UTAWALA WA WAARABU

Ø  Waarabu kutoka Oman walifika Zanzibar na Tanganyika mwishoni mwa karne ya 18. Kwa madhumuni ya kiutawala, walijenga makazi yao katika maeneo ya unguja, pemba na pwani ya Tanganyika, hususani katika miji ya Kilwa, Tanga na Bagamoyo

Ø  Watawala wa kiarabu waliotawala pwani ya Afrika mashariki walifika nchini katika vipindi mbalimbali. Wengi wao walivutiwa na utajiri wa rasilimali uliokuwapo katika eneo hili.

Ø  Utajiri huo ulijulikana kutokana na uhusiano wa kibiashara wa muda mrefu kati ya pwani ya Afrika mashariki na nchi za bara la Asia kama vile Omani, Uhindi, Uchina na Uajemi

Ø  Mtawala wa kwanza katika eneo hili alijulikana kama Sultani Seyyid Said bin Sultan.

·         Sultan alianza kutawala Zanzibar mwanzoni mwa miaka ya 1800

·         Mnano mwaka 1840 Sultan Seyyid Said alihamisha rasmi makao yake kutoka Muscat- Oman hadi Zanzibar na kuifanya Zanzibar kuwa makao makuu ya utawala wake  hadi alipofariki mwaka 1856.

·         Baada ya kifo chake, utawala wake ulirithiwa na watawala wengine kama vile

Ø  Sultan Seyyid Majid

Ø  Sultan Barghash

Ø  Sultan Jamshid bin Abdullah Al Said.

 

 

MAMBO YALIYOMVUTIA SULTAN SEYYID SAID ZANZIBAR.

Sultani alivutiwa sana na;-

i.                    Hali ya hewa ya Zanzibar

ii.                  Kustawi kwa biashara ukanda wa Zanzibar

iii.                Kina kirefu cha bandari ya Zanzibar

iv.                Udongo wenye rutuba uliostawisha mazao kama mikarafuu na minanzi.

 

RAMANI KUONESHA MAENEO AMBAYO WAARABU WALIWEKA NGOME ZA UTAWALA WAO.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Mabadiliko ya kisiasa wakati wa utawala wa Waarabu

Ø  Jamii za pwani ya Tanganyika na Zanzibar zilikuwa na mfumo madhubuti wa uongozi, utoaji wa uamuzi na umiliki wa ardhi kabla ya kuja kwa waarabu wa oman.

Kwa mfano,  ardhi katika jamii nyingi ilimilikiwa kwa pamoja na jamii nzima.

 Baada ya kuja kwa waarabu

Ø  Baada ya kuja kwa waarabu mabadiliko yalitokea. Ardhi yao iliporwa na kugawiwa kwa wakulima wa Kiarabu ili kulima mazao ya biashara ya waarabu.

Ø  Mashamba mengi makubwa yalichukuliwa na waarabu kwa ajili ya kilimo cha minazi na mikarafuu.

Ø  Mtindo mpya wa ugawaji ardhi uliathiri mfumo wa kisiasa wa jadi wa umiliki wa ardhi kwa wanajamii wote, hali iliyosababisha kuibuka kwa matabaka katika jamii.

·         Tabaka la kwanza -lilikuwa la wanyonyaji, likijumuisha viongozi wa serikali, wafanyabiashara wa kihindi na mamwinyi hasa wa kiarabu.

·         Tabaka la pili -lilijumuisha wakulima wadogo wadogo, raia wa kawaida, huku

·         Tabaka la tatu- likiwa la watwana na watumwa.

Ø  Miongoni mwa mbinu walizozitumia waarabu ni kuwagawa watawala wa jadi kwa kumuunga mkono mtawala aliyeonekana kuwa na nguvu zaidi kuliko wenzake na wale walioonekana kuwa wasaliti.

Ø  Kwa upande wa Zanzibar, watawala wa kijadi kama mwinyi mkuu walifanywa kuwa mshiriki mwenza katika utawala.

Ø  Waarabu walitumia uongozi wa mabavu, unyanyasaji na ukandamizaji kwa wananchi.

Ø  Kwa mfano, wananchi walifanyishwa kazi ngumu bila malipo. Walinyang’anywa ardhi yenye rutuba na waafrika wengi walichukuliwa na kupelekwa sehemu zingine kama watumwa.

HIVYO;- Kuja kwa waarabu kulibadilisha mfumo wa utawala kutoka Utawala wa kidemokrasia ya kijadi na umoja  na kuja kwenye utawala wa mabavu, unyanyasaji na ukandamizaji wa wananchi ulioleta mgawanyiko katika jamii.

 

Mabadiliko ya kiuchumi wakati wa utawala wa Waarabu

Kukua kwa biashara ya bidhaa mbalilbali.

Ø  Kuongezeka kwa mahitaji ya pembe za ndovu, karafuu, mafuta ya nazi na mpira katika viwanda vya ulaya na marekani vilimhamasisha sana Sultani wa Zanzibar pamoja na wafanyabiashara wa kiarabu kuendeleza biashaa za bidhaa hizo ikiwemo kuanzisha mashamba makubwa ya mikarafuu na minazi

Ø  Biashara za masafa marefu katika ukanda wa afrika mashariki na kati zilifanyika kwa kutumia njia kuu tatu zilizoanzia pwani kuelekea bara.

a)      Nji ya kaskazini. Nji ya kaskazini ilianzia Saadani kuelekea Pangani hadi mlima Kilimanjaro, kisha kuingia nchini Kenya.

b)      Njia ya kati ilianzia bagamoyo kupitia Morogoro hadi Tabora. Ilipofika tabora, iligawanyika katika matawi mawili: tawi la kwanza lilianzia tabora kuelekea kaskazini huko Karagwe, Buganda na Bunyoro. Tawi la pili lilianzia Tabora kuelekea magharibi huko Ujiji, Burundi, Rwanda, Katanga na Umanyemba huko Kongo. Njia hii ilimilikiwa zaidi na wanyamwezi na wasumbwa.

c)      Njia ya kusini. Njia hii ilianzia Kilwa kivinje kuelekea ziwa Nyasa, Kaskazini mwa msumbiji, Malawi na mashariki mwa Zambia. Njia hii ilitawaliwa na wayao. Njia hizi zilitumika kupitisha bidhaa mbalimbali pamoja na misafara ya watumwa.

Kukua kwa sekta ya kilimo

Ø  Hali kadhalika, waarabu walianzisha mashamba makubwa ya mikarafuu na mpira ili kukidhi mahitaji ya karafuu na mpira katika viwanda vya ulaya na Marekani.

Ø  Mashamba makubwa yaliyoanzishwa yalipelekea ongezeko la mahitaji ya nguvu kazi hasa vibarua wa kupalilia, kuchuma karafuu na kuangua nazi. Hii ilichoichea pia kuanza kwa biashara ya watumwa.

Kuanzishwa kwa biashara ya watumwa.

Ø  Licha ya biashara ya bidhaa mbalimbali iliyofanywa na Waarabu na wenyeji, waarabu hao walianzisha pia biashara ya watumwa.

Ø  Waafrika (watanzania) wengi waliuzwana wengine kutumikishwa katika mashamba makubwa ya mikarafuu na minazi ya waarabu huko visiwani unguja na pemba.

Ø  Pia ukuaji wa kilimo cha miwa huko Komoro, Ngazija, Mauritius na Reunion kulisababisha ongezeko la mahitaji ya watumwa kutoka maeneo mbalimbali hasa Tanganyika.

Kwa ujumla, katika kipindi cha utawala wa waarabu, uchumi ulikuwa wa kinyonyaji, kwani waarabu walikuwa wanufaika wakuu wa mapato, huku waafrika wengi wakinyonywa kwa kufanya kazi kwa ujira mdogo na wengine wakigeuzwa kuwa watumwa.

 

Mabadiliko ya kijamii wakati wa utawala wa Waarabu

Kabla ya kuwasili kwa waarabu, jamii za pwani ya Tanganyika na Zanzibar zilijengwa katika ;-

a)      Maadili yaliyotokana na dini za jadi.

Katika dini za jadi watu waliabudu Mungu kupitia miti mikuwa, mapango makubwa, mito , maziwa na bahari

Pia katika dini za jadi, watu walitoa kafara mbalimbali za wanyama kwa malengo mbalimbali kulingana na imani zao.

b)      Elimu ya jadi.

Elimu ya jadi ililenga kumpatia kijana maarifa na ujuzi wa kukabiliana na mazingira yake.

 

Baada ya kuja kwa Waarabu.

·         Kuja kwa Waarabu kulileta mabadiliko makubwa katika jamii kama ifuatavyo;-

a)      Mabadiliko katika masuala ya elimu.

Watu wengi walianza kujifunza lugha ya kiarabu na kujiunga na madrasa kwaajili ya kujifunza dini ya kiislamu.

b)     Mabadiliko ya kiutamaduni.

Kwa mfano, suala la uvaaji. Uvaaji wa mavazi kama vile kanzu, baibui na baraghashia ulienea sana. Pia lugha ya Kiswahili ilianza kupokea maneno mapya kama vile marhaba, shukrani, sharia .k.

c)      Mabadiliko ya kidini.

Kuja kwa Waarabu kulipelekea watu waachane na dini zao za jadi na kuupokea uislamu. Maadilimya dini za jadi yalionekana kuwa ni ushenzi mbele ya maadili ya dini yaKiislamu.

 

UTAWALA WA WAJERUMANI

Ø Utawala wa wajerumani katika Afrika mashariki ya kijerumani ulisukumwa na mabadiliko ya kiuchumi yaliyojitokeza barani ulaya, ikiwemo nchini Ujerumani. Mabadiliko hayo yalichangiwa kwa kiasi kikubwa na mapinduzi ya viwanda.

Ø Katika robo ya karne ya 19, wajerumani walifika Afrika Mashariki ya kijerumani baada ya kupata taarifa kutoka kwa wamisionari, wafanyabiashara na wapelelezi waliotumwa na wajerumani kuwa malighafi zinapatikana Afrika.

Ø Utawala wa kijerumani katika eneo hili unaweza kugawanywa katika vipindi vifuatavyo:

i)                   Kati ya mwaka 1886 hadi 1891. Kipindi hiki Afrika Mashariki ya Kijerumani ilitawaliwa Kampuni ya Kijerumani ya Afrika Mashariki chini ya mfannyabiashara mjerumani Karl Peters.

ii)                 Kuanzia mwaka 1891 hadi 1918, serikali ya kijerumani ilichukua rasmi mamlaka ya kiutawala.

 

Mbinu walizotumia Wajerumani ili kuimarisha utawala wao katika koloni hili ni;-

è Matumizi ya vyombo vya kiitikadi kama vile elimu na dini

è Matumizi ya vyombo vya dola kama vile jeshi, magereza na mahakama.

è Kuondoa utawala wa jadi kwa kuweka watawala wazungu katika ngazi za uongozi.

 

Mabadiliko ya kiuchumi wakati wa utawala wa Wajerumani

Ujio wa wajerumani ulileta mabadiliko makubwa ya kiuchumi katika jamii za Kitanzania.

a)      Kuanzishwa kwa kilimo cha mazao ya biashara.

Wakati wa utawala wa kijerumani, shughuli za uzalishaji mali zilitegemea sana uzalishaji wa mazao ya biashara kama vile kahawa, chai, mkonge , pamba.k.

 Kwa mfano

·         Kahawa ililimwa Bukoba, Kilimanjaro, Arusha na Tukuyu.

·         Pamba ililimwa Mwanza na Shinyanga

·         Katani (Mkonge) ililimwa Tanga, Morogoro na Lindi

Maeneo mengine kama vile Kigoma, Mtwara, Dodoma na Singida hayakuruhusiwa kuanzisha kilimo cha mashamba makubwa kwaajili ya kutoa wafanyakazi na vibarua katika maeneo waliyoanzisha mashamba.

b)     Uanzishaji wa viwanda vidogovidigo vya kuchakata malighafi.

Wajerumani hawakuanzisha viwanda vikubwa bali walijenga viwanda vidogo, hasa vya kuchakata malighafi ili kupunguza uzito wake kabla ya kusafirishwa kwenda ujerumani.

Kwa mfano. Walijenga vinu vya kukoboa kahawa, kuchambua pamba na kusindika mkonge.

c)      Kuendeshwa kwa biashara ya kinyonyaji.

Wajerumani pia waliendesha biashara ya kinyonyaji, kwani koloni hili lilitumika kama soko la kuuzia bidhaa za viwandani kutoka ujerumani, kama vile nguo, baiskeli, mapanga, majembe, viatu na sigara.

Bidhaa zote hizi ziliuzwa kwa bei kubwa, wakati malighafi zilizotumika kuzalisha bidhaa hizo zilinunuliwa kwa bei ndogo sana.

 

Mabadiliko ya kijamii wakati wa utawala wa Wajerumani

Wajerumani walilazimika kujenga na kutoa huduma kadhaa ili kufanikisha malengo yao. Huduma hizi zilijumuisha elimu, afya, maji na umeme, pamoja na miundombinu ya mawasiliano

(a)   Elimu:

Elimu iliyotolewa na wajerumani ililenga kukidhi mahitaji ya shughuli zao za kikoloni. Walilenga kupata wasaidizi katika shughuli zao. Elimu hiyo ililenga wananchi wachache ambao wangeweza kuzalisha malighafi kwa mahitaji ya viwanda vyao.

Malengo ya elimu hiyo ilikuwa ni;

·         Kueneza utamaduni wa kijerumani

·         Kuandaa watumishi wa ngazi za chini

·         Kufundisha uadilifu na maadili ya kazi

·         Kuandaa wazalishaji mali kwa ajili ya uchumi wa kijerumani

Hivyo mtaala wao ulifundisha stadi kama vile uashi, useremala, ukarani, ufundi kushona na utengenezaji wa viatu.

Kulikuwa na makundi mawili ya shule, shule za wamisionari na shule za serikali.

(b) Afya:

Huduma za afya kipindi cha ukoloni zilitolewa kwa ubaguzi wa rangi, ambapo huduma hizo zilipatikana katika maeneo ambayo wakoloni walianzisha shughuli kubwa za uzalishaji mali kama vile mashamba na makazi yao.

Ø  Wazawa walipata matibabu duni ukilinganisha na wazungu na waasia, na huduma zao zilitilia mkazo kwenye matibabu badala ya kinga za magonjwa.

Ø  Athar hasi za huduma hizi zilikuwa ni kupotea kwa umaarufu kwa waganga na matabibu wa jadi, pamoja na dawa zao kushuka thamani, lakini bado waliendelea kutoa matibabu hasa katika maeneo ya vijijini.

(c) Huduma za maji na umeme:

Katika kipindi cha ukoloni, huduma za maji na umeme zilitolewa kwa ubaguzi na upendeleo, kwani huduma hizi zilielekezwa zaidi katika maeneo yenye umuhimu wa kiuchumi mfano migodini, viwandani, maeneo ya mijini na makazi ya walowezi wa kizungu na kiasia

(d) Miundombinu ya mawasiliano:

Wakoloni walijenga njia za uchukuzi na mawasiliano kama vile barabara, reli na bandari. Hii ilikuwa muhimu kwa usafirishaji wa malighafi, bidhaa na watu.

Reli na barabara zilijengwa kutoka maeneo ya uzalishaji hadibandarini.

 

JAMII ZILIVYOATHIRIKA NA UTAWALA WA WAJERUMANI

i.                    Kuondolewa kwa utawala wa jadi.

Wajerumani walianzisha mfumo wa utawala uliokuwa chini ya liwali na maakida, huku watawala wa jadi wakiondolewa kwa nguvu. Katika baadhi ya maeneo walianzisha utawala wa kijeshi. Hivyo wazawa walipoteza nguvu yao ya kujitawala.

ii.                  Kuanzishwa kwa mfumo wa kulipa kodi.

Wajerumani waliwataka wenyeji kulipa kodi kwa lazima kama vile kodi ya kichwa, lakini wenyeji walikataa. Kwa mfano, Kila raia alitakiwa kulipa kodi ya Rupia tatu. Pale ambapo walikataa au walishindwa kulipa kodi walipewa adhabu kali mfano, kuchapwa viboko hata mbele ya watoto wao.

iii.                Kulipwa ujira mdogo.

Mfano, Wamatumbi wa Kilwa na Wangindo wa Liwale waliathirika kutokana na kulipwa ujira mdogo ukilinganisha na kazi za sulubu walizokuwa wakifanya.

iv.                Kufanya kazi za sulubu.

Kipindi cha utawala wa Wajerumani, wenyeji walilazimishwa kufanya kazi za sulubu kataika miradi mbalimbali iliyoanzishwa na wakoloni. Kazi hizo zilikuwa ni kulima, kuvuna, kusafirisha malighafi n.k. Kazi zilifanyika ka masaa mengi na kwa ujira mdogo na wakati mwingine bila malipo.

v.                  Kutothaminiwa kwa utu wa wanajamii wengi.,

Wazazi au watu wazima walidhalilishwa mbele ya watoto wao.  Kwa mfano,  kuchapwa viboko pale waliposhindwa kulipa kodi ya kichwa au walipotenda makosa madogomadogo.

vi.                Utengano miongoni mwa jamii za Kitanzania.

Utawala wa Kijerumani ulisababisha utengano miongoni mwa jamii za Kitanzania. Kwa mfano, Mangi Maerale wa Wachaga wa Marangu aliungana na Wajerumani kumpiga Mangi Meli wa Moshi.

 

Hitimisho;-

Kwa ujumla jamii za kitanzania zilipata athari katika uchumi na hata kisiasa, kwani mfumo wao wa kujitawala ulibadilishwa. Hali hii iliwapa ujasiri wa kudai uhuru wao kwa nji na mbinu mbalimbali, ikiwemo vita.

 

UTAWALA WA WAINGEREZA TANGANYIKA NA ZANZIBAR

Ø  Mwaka 1919 baada ya vita vya kwanza vya dunia, Afrika mashariki iliyokuwa chini ya Wajerumani ilikabidhiwa kwa Waingereza chini ya udhamini wa jumuiya ya kimataifa (League of Nations) baada ya waingereza kushinda vita hivyo.

Ø  Kwa upande wa Zanzibar, utawala wa waingereza ulianza baada ya kutiwa saini kwa mkataba wa pili kati ya wajerumani na waingereza. Mkataba huo ulisainiwa tarehe 1 julai, 1890, unaojulikana kama mkataba wa Heligoland. Kulingana na mkataba huo, uingereza ilipewa mamlaka ya kuiweka Zanzibar chini ya himaya yake kwa makubaliano na mtawala wa wakati huo, Sayyid Ali bin Said.

Ø  Waingereza walibadili mfumo wa kiutawala uliokuwapo na kuanzisha mfumo wa kiutawala ambao ulibadilisha pia uchumi, siasa na utamaduni wa Tanganyika.

Ø  Jambo muhimu la kufahamu ni kwamba, ni utawala wa kiingereza uliobadilisha jina la koloni hilo kutoka Afrika mashariki ya Kijerumani na kuwa Tanganyika.

 

Mabadiliko ya kiuchumi wakati wa utawala wa Waingereza

Waingereza walilenga kuendeleza kilimo, biashara na viwanda vidogovidogo.

i.                    Kuendeleza na kuhamasisha shughuli za kilimo cha mazao ya biashara.

Kwa upande wa kilimo, walihamasisha kilimo cha mazao ya biashara kam vile kahawa, pamba, mkonge, chai na pareto. Lengo kubwa la kuahamasisha mazao hayo ilikuwa ni kupata malighafi za kutosha kwaajili ya viwanda nchini kwao Uingereza.

ii.                  Kuendelezwaa kwa Shughuli za biashara

Shughuli za biashara zilifanywa na watu wa kiasia, hasa waarabu na wahindi wakati wa ukoloni wa Waingereza. Jamii hii ilijihusisha na biashara ya kununua mazao kutoka kwa wakulima na kuyauza kwa makampuni ya kibepari ya wazungu.

Ø  Pia walifanya biashara ya kuuza bidhaa mbalimbali walizoagiza kutoka ulaya Magharibi na Marekani.

Ø  Watanganyika na wazanzibari hawakuruhusiwa kushiriki katika biashara wakati huo.

iii.                Kuanzishwa kwa viwanda vidogovidoggo

Kwa upande wa viwanda, waingereza hawakuwekeza sana katika viwanda vikubwa ila walianzisha viwanda vodogovidogo.

Ø  Viwanda vidogo vidogo vilivyoanzishwa hapa Tanganyika na Zanzibar vilijikita katika kuchakata malighafi ili kuzipunguzia uzito kabla ya kusafirishwa kwenda ulaya.  

Ø  Kwa mfano, viwanda vya kusindika pamba na kukaushia tumbaku.

iv.                Kufanyika kwa shughuli za usafirishaji na uchukuzi.

Usafirishaji na uchukuzi pia vilipewa kipaumbele na waingereza, walifufua reli pamoja na barabara zilizokuwa zimeathirika kwa vita.

Ø  Pia walikamilisha ujenzi wa reli kutoka Tabora hadi Mwanza.

Ø  Pia bandari na usafiri wa meli katika ziwa Tanganyiaka na Ziwa Victoria uliimarishwa.

v.                  Kuendelezwa kwa shughulu za uchimbaji wa madini.

Waingereza pia waliendeleza uchimbaji wa madini kwa kupanua migodi iliyoachwa na wajerumani na kuanzisha mingine mipya kama migodi ya chumvi huko Uvinza na Ulanga na migodi ya dhahabu huko Chunya na Geita.

 

 

 

Mabadiliko ya kisiasa wakati wa utawala wa Waingereza.

Waingereza waliendelea kutumia mtindo wa utawala uliokuwa unatumiwa na wajerumani. Hata hivyo baadae walibadilisha mfumo wa utawala kama ifuatavyo;-

i.                    Kuanzishwa kwa mfumo wa utawala kwa kuanza kuwatumia viongozi wa jadi

Ø  Waingereza badae walibadilisha mfumo wa utawala kwa kuanza kuwatumia viongozi wa jadi katika shughuli za utawala. Walifanya kazi ya kukusanya kodi, kusimamia maagizo ya serikali, kufanya sensa ya watu na mifugo na kuamua kesi katika mahakama zao.

Ø  Mtindo wa kisiasa wa kuwatumia machifu ulilenga kuwagawa na kuwadhibiti wananchi. Walisisitiza sana ukabila katika mipango yao ili kuondoa hali ya umoja baina yao.

ii.                  Kutungwa sharia na kanuni mbalimbali kwa lengo la kuwakandamiza wananchi.

Ili kuimarisha utawala wa waingereza, sharia na kanuni mbalimbali zilitungwa kwa lengo la kuwakandamiza wananchi.

iii.                Kuunda shirikisho la machifu kwa kila kabila

Waingereza walitumia mbinu za kuwalaghai machifu kwa kuunda shirikisho la machifu kwa kila kabila na kumteua chifu mmoja kuwa kiongozi mwandamizi wa wengine.

Ø  Mfano, Marealle aliteuliwa kuongoza machifu wa kichaga, Makwaia aliteuliwa kuongoza machifu wa kisukuma, Fundikira aliteuliwa kuongoza machifu wa Kinyamwezi n.k.

iv.                Kupanua baraza la kutunga sharia.

Baraza hili lilijumuisha machifu wa Kitanganyika wakiwemo Chifu Abdieli Shangali na Chifu Kidaha Makwaia. Majukumu ya baraza hili yalikuwa ni

Ø  Kutunga sharia ambazo zilihitaji idhinikutoka serikali ya Uingerza kabla ya kutumika

Ø  Kumshauri Gavana masuala mbalimbali yanayohusu utawala

 

v.                  Kuanzishwa kwa baraza la ushauri Zanzibar.

Kwa upande wa Zanzibar, Waingereza walianzisha baraza la ushauri mnamo mwaka 1914 kwa lengo la kumshauri Sultani na serikali yake kuhusu masuala ya serikali.

Ø  Unguja na Pemba ziligawanywa katika wilaya, Mudiria na Shehia. Katika Wilaya kulikuwa na Afisa  mtawala wa Kiingereza huku Mudir na Sheha wa kiarabu wakisimamia Mudiria na Shehia.

Ø  Pia kulikuwa na Waafrika wachache waliokuwa wakisimamia Shehia lakini walipewa jukumu la kuwahimiza wenzao kuwatumikia Waarabu, Wazungu na Wahundi.

 

Mabadiliko ya kijamii wakati wa utawala wa Waingereza

Ø  Mabadiliko ya kijamii wakati wa utawala wa waingereza yalijikita zaidi katika utoaji wa huduma za msingi kama elimu, afya, maji, umeme na miundombinu.

Ø  Huduma hizi zilitolewa kwa madhumuni ya kuiwezesha serikali ya Waingereza kurahisisha utekelezaji wa malengo ya kikoloni.

i.                    Elimu:

Shughuli za utoaji wa elimu ziliathirika sana wakati wa vita kuu ya kwanza ya Dunia. Serikali ya Uingereza, kwa kushirikiana na mashirika ya dini, ilianza kutoa elimu kwa wananchi kwa kufuata mipango na mahitaji ya wakoloni.

Ø  Sehemu zilizopewa kipaumbele ni zile zilizozalisha mazao ya biashara kama vile Kilimanjaro na Bukoba

Ø  kwa upande wa Zanzibar, waingereza walitoa elimu iliyoendeleza matabaka ya kijamii.

Ø  Wazanzibari walifundishwa jinsi ya kuwa watiifu na waaminifu kwa sultani na viongozi wao, ambao wengi walikuwa waarabu.

Ø  Waarabu walipewa elimu maalumu iliyowafanya waendelee kujiona kuwa bora kuliko waafrika.

ii.                  Afya:

Huduma za afya wakati wa utawala wa Waingereza zilitolewa kwa lengo la kuziendeleza na kuzilinda afya za wananchi ili wawe na nguvu za kushiriki kikamilifu katika shughuli za kuendeleza uchumi wa kikoloni.

Ø  Pamoja na kwamba walihitaji nguvukazi yenye afya, bado huduma za afya zilikuwa chache na duni.

Ø  Lakini pia huduma za afya zilitolewa kwa ubaguzi mkubwa sana. Kwa mfano, huduma bora zaidi zilitolewa kwa Wazungu, wakifuatiwa na Waasia huku Waafrika wakipewa huduma za chini.

Ø  Hospitali pia zilikuwa na mfumo wa ubaguzi. Kwa mfano Hospitali ya Ocean Road ( Dar es salaam) ilikuwa maalumu kwa Wazungu kwakuwa ilitoa huduma bora zaidi.

 

iii.                Miundombinu:

Katika kutekeleza mpango wa ukoloni wa kupata malighafi muhimu kwa ajili ya viwanda ulaya, waingereza waliendelea kufufua na kuanzisha miundmbinu kutoka maeneo ya pwani hadi maeneo ya uzalishaji mali kama migodi na mashamba ya pamba, mkonge na kahawa.

Ø  Miundombinu iliyojengwa ni pamoja na barabara, reli na bandari.

Ø  Kwa mfano, Relimkutoka Tabora hadi Mwanza ilikamilishwa mwaka 1928.

Ø  Bandari za Tanga na Dar es salaam zilikarabatiwa pia walijenga bandari ya Mtwara.

iv.                Huduma za maji na umeme:

Serikali ya uingereza ilijitahidi kuwapa wananchi wa Tanganyika na Zanzibar huduma za maji na umeme ili kuwawezesha kuwa na afya bora ili kuendelea kuzalisha malighafi.

Ø  Baada ya vita kuu vya pili vya dunia, serikali ilipanua huduma hizi katika maeneo ya mashamba, migodini na mahali walipoishi watawala wa kikoloni.

Ø  Huduma hizi zilikuwa pia za kibaguzi. Kwa mfano, huko mijini huduma bora za maji na umeme walipewa kwanza Wazungu wakifuatiwa na Wasia na Waafrika.

Ø  Maeneo ya vijijini yaliendelea kutumia kuni, koroboi na taa za chemli ili kupata mwanga wakati za usiku.

 

MCHANGO WA UKOLONI KATIKA UHUSIANO WA TANZANIA NA MATAIFA YALIYOITAWALA

v  Kabla ya ujio wa wakoloni, jamii za kitanzania zilikuwa na uhusiano wa kuheshimiana na kushirikiana na jamii nyingine za afrika na kwingineko.

v  Uhusiano huu ulijengwa kwa misingi ya biashara, ambapo jamii zilibadilishana bidhaa kama vile dhahabu, pembe za ndovu na vyakula. Ushirikiano huu ulizingatia maadili ya kutegemeana, kusaidiana na kuaminiana.

v  Biashara iliyofanyika kati ya jamii hizi ilichangia kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi

 

Hali hii ya ushirikiano ilianza kubadilika baada ya ujio wa wakoloni kutoka ulaya magharibi.

i.                    Rasilimali za watanzania zilinyonywa kama vile ardhi na madini

ii.                  Kuvunja uhusiano wa asili na kuanzisha  mipaka mipya

iii.                Kuanzishwa kwa  sera mpya zilizoharibu maadili ya kijamii ya kitanzania.

iv.                Utamaduni wa kigeni ulienea katika jamii za kitanzania na kudhoofisha utamaduni na maadili ya asili.

v.                  Kuvunjika kwa mshikamano wa kijamii na kuendeleza uhusiano hasi kati ya jamii za kitanzania na wakoloni

vi.                Kuongezeka kwa uhasama na migongano kati ya wakoloni na wazawa. Hii ilitokana na kutumia mbinu za kijeshi na kisiasa katika kuwatawala Watanzania.

 

HIVYO;-

v  Ukoloni ulisababisha mwamko mpya wa kudai uhuru. Harakati za kudai uhuru na kujikomboa zilichochea umoja miongoni mwa jamii za kitanzania.

v  Baada ya Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961, uhusiano mpya ulijengwa kati ya Tanganyika na mataifa ya kigeni, yakiwemo mataifa yaliyokuwa yanaitawala.

v  Katika kipindi hicho cha uhuru wa Tanganyika na mara baada ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Tanzania ilijipambanua kama taifa lenye msimamo huru katika uhusiano wake na mataifa mengine.

 

 

 

 

ZOEZI

1. Eleza sababu za wakoloni kutoanzisha viwanda vya kuzalisha bidhaa katika maeneo ya Tanzania wakati wa ukoloni

2. Linganisha hali ya utoaji wa huduma za jamii wakati wa utawala wa wajerumani na waingereza katika jamii za kitanzania

3. Fafanua namna ambavyo sera za utawala wa wajerumani na waingereza zilivyokinzana na maadili ya jamii za kitanzania

4. Jamii za sasa za Tanzania zinaweza kujifunza ninikuhusu usimamizi wa rasilimali na utawala kutoka kwa wajerumani na waingereza?

5. Kwa kurehelea utoaji wa huduma za jamii wakati wa ukoloni, pendekeza namna bora ya kuboresha utoaji wa huduma za kijamii katika Tanzania ya sasa

6. Tofautisha utoaji huduma za jamii wakati wa sasa na ule wa utawala wa wajerumani na waingereza 


No comments:

Post a Comment