FORM ONE: MADA YA PILI

CHIMBUKO LA JAMII ZA KITANZANIA NA MAADILI YAKE

Mwanzo
Asili ya jamii za Kitanzania inatokana na historia ya muda mrefu ya makabila mbalimbali yanayoishi nchini Tanzania. Katika sehemu hii, utajifunza chimbuko la jamii za Kitanzania kwa kuzingatia nadharia tofauti, mtawanyiko wa jamii hizo katika maeneo mbalimbali ya kijiografia, pamoja na shughuli zao za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Vilevile, utajifunza maadili ya jamii za asili za Kitanzania na uhusiano uliopo kati ya jamii hizo na jamii za mataifa mengine. Umahiri utakaojengeka utakuwezesha kuthamini na kuzingatia maadili ya jamii za Kitanzania pamoja na kuishi vyema katika jamii yako.

Dhana ya Jamii

Wanazuoni na wanafalsafa mbalimbali wamefafanua dhana ya jamii kwa namna tofauti. Kwa mfano, mtaalamu Emile Durkheim (1884) anaeleza kuwa jamii ni mkusanyiko wa watu kwa ujumla wake. Kwa mujibu wa mwanazuoni huyu, mtu ndiye kichocheo cha maendeleo ya jamii. Kwa upande mwingine, Margaret Thatcher (1987) anafafanua jamii kuwa ni watu, yaani wanaume, wanawake na familia zao. Aidha, mwanafalsafa Jean Jacques Rousseau (1797) anaeleza kuwa jamii ni jumla ya watu mmoja mmoja. Hivyo, ni wazi kuwa wanazuoni hawa wote wanakubaliana kwamba jamii ni watu. Katika muktadha huo, jamii ni mkusanyiko wa watu uliotokana na historia kwa lengo la kuendeleza maisha yao na shughuli za uzalishaji. Historia inaonesha kuwa tangu zamani, watu wamekuwa wakiishi pamoja huku wakidumisha upendo, amani, umoja na mshikamano katika jamii. Jamii huishi katika vijiji, miji, nchi na mataifa kupitia shughuli mbalimbali kama uwindaji, kilimo, uvuvi, ufugaji na biashara. Jamii huundwa na makundi tofauti. Kundi la kwanza ni watu wenye uhusiano wa damu au ndoa linaloitwa familia. Familia ni kikundi kidogo cha watu wenye uhusiano wa damu au ndoa kinachojumuisha baba, mama, watoto na ndugu wengine wa baba au mama. Familia kadhaa zenye asili moja na uhusiano wa damu huunda kundi linaloitwa ukoo. Kila ukoo huwa na kiongozi wake. Ukoo kadhaa wenye uhusiano huunda kundi kubwa zaidi linaloitwa kabila. Kabila ni kundi la watu wanaozungumza lugha moja na wenye mila na desturi zinazofanana. Jamii za Kitanzania zimepitia hatua mbalimbali za mabadiliko na maendeleo kuanzia ujima, ukabaila, ubepari hadi ujamaa. Maendeleo hayo yalisababisha mgawanyo wa kazi na kuibuka kwa matabaka mbalimbali katika jamii. Kwa hiyo, ni muhimu kujifunza asili ya jamii za Kitanzania ili kufahamu tulikotoka na mahali tulipo sasa.

Asili Ya Jamii Ya Kitanzania

Jamii za Kitanzania zinajumuisha makabila mbalimbali yenye tofauti katika mwonekano, asili, tabia pamoja na shughuli za kijamii na kiuchumi. Licha ya tofauti hizo, jamii hizi zote huishi pamoja kwa mshikamano. Hali hii ina historia yake ambayo ni muhimu kuielewa kwa ajili ya kudumisha umoja, kulinda amani, na kuendeleza maslahi ya Taifa letu kwa sasa na siku zijazo. Ni muhimu kufahamu historia ya asili ya jamii zetu, mtawanyiko wake, na namna jamii hizo zilivyoweza kuishi pamoja kwa amani. Ni dhahiri kwamba taifa la Tanzania halikutokea kwa bahati mbaya, bali ni matokeo ya mchakato mrefu wa kihistoria. Hivyo, tunapaswa kuelewa kwamba Tanzania ya leo ni zao la maendeleo ya jamii yaliyotokea katika vipindi mbalimbali vya historia. Vilevile, ni muhimu kutambua kuwa Tanzania ni nchi ya kipekee duniani kwa upande wa historia. Hii ni kutokana na ukweli kwamba ina zaidi ya makabila 150. Kwa kuzingatia uchambuzi wa makabila, Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye makundi yote makuu ya makabila yanayopatikana barani Afrika (Kielelezo 2.1). Makundi hayo ni Wabantu, Wakhoisan, Wakushito na Wanilo.
(Source: TIE) Kielelezo 2.1: Chimbuko la makundi makuu ya jamii za Kitanzania

Wabantu ni kundi linalojumuisha jamii nyingi za Watanzania wa leo ambao wamesambaa katika eneo kubwa nchini. Takwimu zinaonesha kwamba jamii za Wabantu zinakadiriwa kufikia asilimia 75 ya Watanzania wote. Chimbuko la Wabantu wa Tanzania ni Afrika Magharibi katika eneo lililopo kati ya nchi za Kameruni na Nijeria. Kati ya kipindi cha miaka 3000 kabla ya zama za sasa, Wabantu walisambaa Afrika hasa kusini mwa Jangwa la Sahara hadi kusini mashariki mwa Bara la Afrika. Mfano wa jamii za Wabantu nchini Tanzania ni Wachaga, Wagogo, Waha, Wahadimu, Wahehe, Wakurya, Wamakonde, Wangoni, Wanyakyusa, Wanyamwezi, Wapemba, Wasukuma, Watumbatu, Wayao na Wazaramo. Kwa mfano, Watumbatu wanapatikana kaskazini mwa kisiwa cha Unguja, kisiwa cha Tumbatu, Nungwi, Mkokotoni, Mahonda na kwingineko. Wahadimu wanapatikana kusini na mashariki ya Kisiwa cha Unguja katika maeneo ya Chwaka, Bwejuu, Makunduchi, Kizimkazi na Uzi.  Kundi lingine la jamii za Kitanzania ni Wakichembe ambao kwa asili ni wawindaji. Jamii hii ndio watu wa asili wa eneo ambalo sasa ni Tanzania. Wakichembe walikuwapo kwa miaka mingi kabla ya ujio wa Wabantu. Jamii zinazounda kundi la Wakichembe ni Wasandawe na Wahadzabe wanaopatikana katika Bonde la Ufa katikati ya Tanzania na kandokando ya Ziwa Eyasi. Jamii ya Wakushito ni kundi lingine la Watanzania linajumuisha makabila ya Waalawa, Wagorowa na Wairaki. Kiasili, Wakushito ni Waafroasiatiki kutoka maeneo ya Pembe ya Afrika katika nchi za Ethiopia, Eritria na Somalia.  Kihistoria Wanilo ni kundi kubwa la tatu la Watanzania ambalo ni jamii ya wafugaji walioingia nchini Tanzania wakitokea kusini mwa Sudani. Wanilo ni watu wa asili ya Bonde la Mto Naili ambao wanatumia lugha ya Kinilo. Jamii hii imetawanyika katika nchi za Sudani, Ethiopia, Sudani Kusini, Kenya, Uganda na Tanzania. Mfano wa jamii za Wanilo ni Wamasai, Waluo na Wadatoga, ambao wanajumuisha makabila ya wafugaji. Kielelezo 2.2  kinaonesha picha za watu wa jamii za Wakichembe (A), Wakushito (B), na Wanilo (C).
(Source: TIE) Kielelezo 2.2: Watu wa jamii ya Wakichembe, Wakushito na Wanilo
Makundi haya yanajumuisha jamii ya Watanzania na yamekuwapo kwa zaidi ya miaka 500 iliyopita. Asili na sababu za jamii hizi kuishi Tanzania ni za kihistoria.

KAZI YAKUFANYA

  1. Kwa nini ni muhimu kuelewa historia ya asili ya jamii za Kitanzania na jinsi zilivyoishi pamoja kwa amani?
  2. Tanzania inatajwa kuwa nchi ya kipekee kihistoria duniani kwa sababu gani?
  3. Taja makundi makuu manne ya jamii za Kitanzania yaliyotajwa katika matini.
  4. Wabantu walitokea katika eneo gani la Afrika kabla ya kusambaa katika sehemu mbalimbali za bara hilo?
  5. Ni jamii zipi zinazounda kundi la Wakichembe na zinapatikana katika maeneo gani nchini Tanzania?
  6. Wanilo walitokea wapi na ni makabila gani ya Wanilo yaliyotajwa katika matini?
  7. Je, tofauti za makabila mbalimbali nchini Tanzania zinachangiaje mshikamano wa Taifa?
  8. Unafikiri ni mambo gani yamewezesha jamii mbalimbali za Tanzania kuishi pamoja kwa amani kwa muda mrefu?
  9. Mtawanyiko wa jamii za Tanzania kabla ya ukoloni

    Wakichembe:
    Wakichembe ni jamii ya watu waliokuwa wameenea Afrika kabla ya kutokea kwa mtawanyiko wa Wabantu. Kwa asili, jamii hii ndiyo wazawa wa kwanza wa eneo lililokuwa Tanganyika. Jamii hii hutumia lugha ya Kichembe inayojulikana kwa matumizi ya sauti za kugongagonga ulimi. Shughuli zao kuu za kiuchumi ni uwindaji na ukusanyaji wa matunda porini. Mifano ya jamii hizi ni Wahadzabe na Wasandawe. Wahadzabe waliishi katika eneo la Ziwa Eyasi, huku Wasandawe wakipatikana kaskazini mwa Ugogo. Ingawa kwa sasa jamii hizi zimechangamana na tamaduni za jamii jirani, bado zinaendelea kuhifadhi sehemu kubwa ya utamaduni wao.
    Wakushito:
    Wakushito wanaoishi Tanzania ya leo ni sehemu ya Wakushito wa kusini mwa Jangwa la Sahara, ambapo wengi wao ni Wairaki na Wagorowa. Jamii hizi ni sehemu ya kundi lenye mchanganyiko wa asili ya Kiafrika na Kiasia. Chimbuko lao ni Ethiopia, na shughuli zao kuu za kiuchumi ni kilimo na ufugaji. Wakushito walihamia kusini mwa Bonde la Ufa katika karne ya 3 Kabla ya Zama za Sasa. Takribani miaka 1000 baada ya Zama za Sasa, walisogea kuelekea kaskazini mwa Tanzania wakitafuta maeneo bora ya kilimo na malisho ya mifugo.
    Wanilo:
    Wanilo wa Tanzania ya leo ni sehemu ya jamii za Wanilo wa kusini wanaopatikana Afrika Mashariki, hususan Tanzania, Uganda na Kenya. Wanilo wamegawanyika katika makundi mengi madogo kuliko Wabantu. Kwa ujumla, jamii hizi zinajumuisha Wadatoga na Wamasai. Kundi kubwa zaidi la Wanilo nchini Tanzania ni Wamasai. Aidha, Wanilo wamegawanyika katika makundi mbalimbali kama Wagisarajengi, Wabarabaigi, Waiseimajegi na Wairudageingi wa Bonde la Ruwana, Musoma. Pia wapo Waburadigi, Wabajudi na Wadagwajegi wanaoishi eneo la Ziwa Eyasi kusini mwa Mto Sibiti. Makundi mengine ni Waghumbiegi, Wamangadigi, Wadaragwajegi, Wablanjidi na Wareiraojigi wanaoishi kandokando ya Mto Werabere kusini mwa Itigi mkoani Singida. Kundi jingine ni Wataturu wanaoishi katika eneo la Itigi.
    Licha ya kupokea athari za kiutamaduni kutoka kwa Wakushito, hasa Wairaki, makundi mengi ya Wanilo yameendelea kuhifadhi utamaduni wao isipokuwa Wagisamjengi. Jamii hizi pia zimeathiriwa kwa kiasi fulani na Wakushito na Wabantu. Wadatoga wengi wanaishi katika maeneo yanayofaa kwa ufugaji, jambo linalowasaidia kuendeleza maisha yao ya ufugaji badala ya kilimo. Kwa kuwa walikuta maeneo ya mbuga na Bonde la Ufa tayari yamekaliwa na Wabantu na Wakushito, Wanilo walitumia nguvu kupata maeneo ya makazi na malisho. Hali hii ilisababisha kuwa na mfumo wa kijeshi uliozingatia uongozi wa kirika. Hata hivyo, Wanilo wamepitia mabadiliko mengi ya kijamii, kiutamaduni, kisiasa na kiuchumi. Kwa sasa, baadhi yao hujihusisha na kilimo, ingawa kwa kiwango kidogo. Ingawa hawajaandikwa sana katika machapisho ya historia ya Tanzania, mchango wao katika kuhifadhi utamaduni wa Mtanzania ni mkubwa tangu Milenia ya Kwanza ya Zama za Sasa.
    Wabantu:
    Kwa asili, Wabantu walihama kutoka eneo lililopo kati ya Kameruni na Nigeria na kusambaa kuelekea kusini na mashariki mwa Afrika. Walipofika, waliwakuta wenyeji waliokuwa wawindaji na wakusanyaji. Kutokana na idadi yao kuwa kubwa, waliingiza taratibu utamaduni na lugha zao kwa hiari au kwa ushawishi mkubwa. Katika safari yao ya uhamaji, walivuka milima, mabonde na misitu ya Kongo. Walifuata matawi ya Mto Kongo kutoka Kameruni kupitia Ubangi-Shari hadi nyanda za kusini mwa misitu ya Kongo. Kutoka hapo, waliendelea kusambaa hadi Afrika Mashariki, ikiwemo Tanzania, katika kipindi cha Milenia ya Kwanza ya Zama za Sasa.
    Ujasiri, uthubutu na uvumilivu wao katika safari hizo ni jambo la kuvutia. Wabantu walitawanyika kutokana na sababu mbalimbali. Kwanza, kulikuwa na migawanyiko ya koo iliyosababishwa na mahitaji ya maisha kama chakula na makazi. Pili, mabadiliko ya hali ya hewa kama ukame yaliathiri shughuli za kilimo na ufugaji. Tatu, walitafuta ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kilimo na malisho ya mifugo. Mtawanyiko huu uliwezesha mchanganyiko wa jamii na maendeleo katika kilimo, matumizi ya chuma, viwanda na biashara ya kubadilishana bidhaa. Wabantu wa pwani waliathiriwa na utamaduni wa wageni, hususan Waarabu waliofika baada ya karne ya 7. Ujio wao uliathiri mila, desturi na ustaarabu wa Wabantu wa pwani, ambao baadaye walijulikana kama Waswahili.
    Wahadimu:
    Wahadimu ni jamii ya Wabantu wanaopatikana katika maeneo ya kati na kusini mwa Kisiwa cha Unguja. Neno Hadimu limetokana na neno la Kiarabu hudma lenye maana ya kutoa huduma. Watu waliokaa maeneo hayo walikuwa chini ya utawala wa Mwinyi Mkuu na walifanya kazi kwa niaba yake au kwa niaba ya Sultani. Kutokana na hali hiyo, walikuja kujulikana kama Wahadimu. Maeneo yao makuu ni Makunduchi, Paje, Bambi, Uroa, Chwaka na Dunga. Pia, baadhi yao wanapatikana katika maeneo ya kaskazini mwa Unguja.
    Watumbatu:
    Watumbatu ni watu waliohamia na kuishi katika Kisiwa cha Tumbatu pamoja na maeneo ya kaskazini mwa Unguja. Kulingana na historia, wageni waliofika Zanzibar katika karne ya 11 waliwakuta watu wa Unguja ambao baadaye walihamia Kisiwa cha Tumbatu. Kwa asili, Watumbatu ni Wabantu. Wanajitambulisha kupitia utamaduni na lugha yao, ambayo ni sehemu ya lahaja za Kiswahili zinazozungumzwa Zanzibar. Kiongozi wao wa jadi alijulikana kama Mwana wa Mwana.
    Wapemba:
    Wapemba ni watu waliohamia na kuishi katika Kisiwa cha Pemba tangu karne nyingi zilizopita. Mwingiliano kati yao na wageni waliowasili katika pwani ya Afrika Mashariki ulisababisha mchanganyiko mkubwa wa rangi katika jamii ya Wapemba kuliko ilivyo kwa Unguja. Wapo Wapemba wa kusini na wa kaskazini ambao huzungumza Kiswahili chenye lafudhi na viimbo tofauti. Maeneo kama Kiuyu, Micheweni, Tumbe, Gando, Kangagani, Chake Chake, Kojani na Mkanyageni yanaonesha mchanganyiko mkubwa wa jamii kutoka nje ya Bara la Afrika. Kiongozi maarufu wa jadi wa Wapemba alijulikana kama Mkama Ndume. Pamoja na jamii hizi za Kibantu, kuna jamii ya Washirazi katika visiwa vya Zanzibar. Washirazi walitoka Ghuba ya Uajemi kwa kutumia majahazi na ndio walioanzisha kizazi cha Kishirazi katika mwambao wa Afrika Mashariki. Kiongozi wao aliitwa Mwinyi Mkuu. Sababu kuu za kuwasili kwao zilikuwa biashara na kukimbia migogoro ya kugombea madaraka katika jamii za Waajemi. Kuna Washirazi wa Unguja na Washirazi wa Pemba.

    Matokeo ya Uhamaji

    Uhamaji ni kitendo kinachohusisha mtu binafsi, familia, kundi la watu au jamii nzima kuondoka eneo moja la makazi na kwenda kuishi katika eneo jingine. Uhamaji ni sehemu muhimu ya historia ya binadamu na umekuwapo tangu nyakati za kale. Watu wamekuwa wakihama kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa lengo la kuboresha maisha yao au kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maeneo yao ya asili. Uhamaji unaweza kuwa wa muda mfupi au wa kudumu kulingana na sababu zinazowafanya watu kuhama. Kuna sababu mbalimbali zinazochangia uhamaji wa watu. Baadhi ya sababu hizo ni za kijiografia kama vile ukame, mafuriko, milipuko ya magonjwa na majanga mengine ya asili yanayofanya maeneo fulani yasifae kwa makazi ya binadamu. Sababu za kiuchumi pia zimekuwa na mchango mkubwa katika uhamaji wa watu, hususan kutafuta ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kilimo, malisho ya mifugo, biashara na ajira. Aidha, sababu za kisiasa kama vita, migogoro ya kikabila, ukandamizaji wa kisiasa na kutafuta usalama zimewalazimu watu wengi kuhama kutoka maeneo yao ya asili. Vilevile, sababu za kijamii na kiutamaduni kama vile ndoa, elimu na kuungana na ndugu au jamaa zimechangia uhamaji wa watu katika maeneo mbalimbali. Barani Afrika, uhamaji umekuwa sehemu ya maisha ya kila siku kwa karne nyingi. Tofauti na maeneo mengine duniani ambapo wahamiaji wakati mwingine hukataliwa au kubaguliwa, katika jamii nyingi za Kiafrika wahamiaji walipokelewa kwa ukarimu na kupewa nafasi ya kuishi pamoja na wenyeji. Wahamiaji walikubaliwa kuwa sehemu ya jamii mpya na walishiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kisiasa. Huu ni utamaduni wa Kiafrika uliojengwa juu ya misingi ya ujamaa, mshikamano, ushirikiano na kuheshimiana. Utamaduni huu umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha amani na umoja katika jamii nyingi za Afrika, ikiwemo Tanzania. Nchini Tanzania, mwingiliano kati ya wahamiaji na wenyeji umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha maadili ya kijamii kama vile upendo, uvumilivu, mshikamano, ushirikiano na amani. Jamii mbalimbali zilipokutana kutokana na uhamaji, zilibadilishana tamaduni, maarifa, lugha na mbinu za uzalishaji mali. Matokeo yake yalikuwa kuibuka kwa jamii zilizoishi kwa pamoja licha ya tofauti zao za kikabila na kitamaduni. Hali hii imeifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zenye amani na umoja mkubwa barani Afrika. Mfano mzuri wa matokeo ya uhamaji ni kuwasili kwa Waluo katika mkoa wa Mara. Waluo walianza kuhamia eneo hilo kupitia Kenya kuanzia karne ya 16 ya Zama za Sasa. Uhamaji huo uliendelea katika karne ya 19 na hata mwanzoni mwa karne ya 20. Walipofika katika maeneo ya Mara, waliwakuta Wasuba ambao ni jamii ya Kibantu iliyokuwa imeishi katika eneo hilo kwa muda mrefu. Badala ya kuzuka migogoro mikubwa kati ya jamii hizo mbili, kulijengwa mahusiano ya amani na ushirikiano yaliyochangia maendeleo ya eneo hilo. Mahusiano hayo yaliimarishwa kupitia mwingiliano wa kijamii na kifamilia. Baadhi ya viongozi wa Kijaluo, hususan machifu na watu waliokuwa na mifugo mingi, walioa wanawake kutoka jamii ya Wasuba. Ndoa hizi zilisaidia kuunganisha jamii hizo na kuimarisha mshikamano kati yao. Watoto waliozaliwa katika familia hizo walikuwa kiungo muhimu kati ya jamii hizo mbili na walichangia kuondoa tofauti zilizoweza kujitokeza. Aidha, jamii za Waluo na Wasuba zilianzisha mifumo ya pamoja ya uongozi na ulinzi wa jamii. Walikuwa na kamati za wazee zilizokuwa na jukumu la kusimamia amani, kutatua migogoro na kuhakikisha haki inatendeka kwa wanajamii wote bila ubaguzi. Wazee hao waliheshimiwa na jamii zote na maamuzi yao yalizingatiwa na kila mtu. Mfumo huu wa jadi wa utawala ulisaidia kuzuia migogoro na kuimarisha mshikamano wa kijamii. Kwa ujumla, historia ya uhamaji nchini Tanzania inaonesha kuwa watu kutoka jamii tofauti wanaweza kuishi pamoja kwa amani, kuheshimiana na kushirikiana katika kujenga maendeleo ya pamoja. Uhamaji umechangia kuunda taifa la Tanzania lenye mchanganyiko wa makabila na tamaduni mbalimbali lakini lenye umoja, mshikamano na amani inayodumu hadi leo. Kupitia uhamaji, Watanzania wamejifunza umuhimu wa kuvumiliana, kuheshimiana na kuthamini tofauti zao kama msingi wa maendeleo ya taifa.

    Shughuli za makundi ya asili ya jamii za Kitanzania

    Shughuli za Kijamii, Kiuchumi na Kisiasa za Jamii za Asili za Tanzania Makundi ya asili ya jamii za Kitanzania, kama ilivyo kwa jamii nyingine za Afrika na sehemu mbalimbali za dunia, yalijihusisha na shughuli nyingi za kijamii, kiuchumi na kisiasa. Shughuli hizo zilichangia maendeleo ya jamii husika kulingana na mazingira yao. Wafinyanzi, wafumaji, wahunzi na wafanyabiashara walibadilishana bidhaa mbalimbali kama chumvi, shaba, chuma na mazao mengine ili kupata mahitaji yao ya kila siku. Mwingiliano huu ulisaidia kukuza uchumi na kuimarisha mahusiano kati ya jamii tofauti. Jamii za Kibantu Jamii za Kibantu zilijishughulisha na shughuli mbalimbali za uzalishaji mali kama kilimo, ufugaji na uvuvi. Shughuli hizi zilitegemea mazingira ya maeneo waliyoishi. Kutokana na matumizi ya zana za chuma, waliweza kulima mazao mbalimbali kama mtama, uwele, viazi vikuu na mazao mengine ya mizizi. Katika maeneo yenye mvua nyingi walifanya kilimo cha kudumu, huku maeneo yenye ardhi kubwa yakitumia mfumo wa kilimo cha kuhamahama. Mbali na kilimo, Wabantu walifuga ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku. Ufugaji uliwapatia chakula, ngozi na mali ya kujivunia. Katika maeneo yenye mito, maziwa na bahari walifanya shughuli za uvuvi kwa kutumia mitumbwi, nyavu na mitego ya asili iliyotengenezwa kwa matete na miti. Kisiasa, jamii za Kibantu zilikuwa na mfumo wa utawala wa kiukoo. Familia na ukoo vilikuwa msingi wa utawala. Kiongozi wa ukoo alikuwa na jukumu la kusimamia mashamba, mifugo, misitu, sherehe za kidini, ndoa na kutatua migogoro. Ili mtu awe kiongozi alipaswa kuwa jasiri, mwenye busara, mjuzi wa mila na desturi pamoja na kuwa na uwezo wa kuongoza watu. Kijamii, jamii hizi zilitoa elimu ya jadi kupitia jando na unyago. Vijana wa kiume walifundishwa uwajibikaji, uongozi, maadili mema na mbinu za kujitegemea. Wasichana walifundishwa majukumu ya kifamilia, malezi na maisha ya ndoa. Huduma za afya zilitegemea waganga wa jadi waliotumia mitishamba na matambiko kutibu magonjwa mbalimbali. Aidha, shughuli kama ususi, uhunzi, ufinyanzi, ushonaji na ujenzi zilikuwa sehemu muhimu ya maisha yao ya kila siku. Jamii za Visiwa vya Zanzibar Jamii nyingi za Zanzibar zina asili ya Kibantu. Miongoni mwao ni Wahadimu, Watumbatu na Wapemba. Kutokana na biashara ya baharini, Zanzibar ilivutia wageni kutoka Uarabuni, Uajemi, India na maeneo mengine ya dunia, jambo lililosababisha kuibuka kwa makundi kama Washirazi. Shughuli kuu za kiuchumi zilikuwa kilimo, uvuvi na biashara. Mazao makuu yalikuwa karafuu, iliki, pilipili na mazao mengine ya viungo. Wafanyabiashara wa Zanzibar walifanya biashara na nchi za Uarabuni, Uajemi, China, Indonesia na Ulaya. Bidhaa zilizouzwa nje ni pamoja na karafuu, pembe za ndovu, nta na dhahabu, huku bidhaa kama nguo, manukato na silaha zikiingizwa kutoka nje. Jamii hizi zilijulikana kwa maadili ya uaminifu katika biashara. Wafanyabiashara wakubwa waliwakopesha bidhaa wafanyabiashara wadogo kwa makubaliano ya kulipa baada ya kuuza bidhaa hizo. Pia viongozi wao walitumia mali kwa manufaa ya jamii nzima. Wakati wa njaa, chakula kilichohifadhiwa katika maghala ya viongozi kiligawiwa kwa wanajamii waliokuwa na mahitaji. Jamii za Wakichembe Wakichembe ni miongoni mwa jamii za kale zaidi nchini Tanzania na huaminika kuwa wakazi wa mwanzo wa eneo hili. Jamii hizi ziliishi kwa uwindaji wa wanyama kama swala, digidigi na wanyama wengine wadogo. Pia walikusanya matunda, mizizi, asali, mayai ya ndege na vyakula vingine kutoka misituni. Wakichembe hawakuwa na makazi ya kudumu. Walihamahama wakifuata maeneo yenye chakula na maji. Walitumia mapango, chini ya miti mikubwa na vibanda vya muda kama makazi yao. Katika uwindaji walitumia mikuki, mishale, mawe na mifupa ya wanyama. Mfano wa jamii za Wakichembe ni Wahadzabe na Wasandawe. Elimu ilitolewa kwa vitendo ambapo watoto walijifunza kutoka kwa wazazi na watu wazima. Viongozi walichaguliwa kulingana na shughuli maalumu kama uwindaji na hawakuwa viongozi wa kudumu. Maadili yao yalisisitiza matumizi endelevu ya rasilimali. Hawakuua wanyama wote bali waliwaacha baadhi kwa ajili ya kuzaliana. Pia walishirikiana na jamii za jirani kwa kubadilishana bidhaa kama asali kwa mikuki ya chuma au mazao ya kilimo. Jamii za Wakushito Jamii za Wakushito zinajumuisha Wairaki, Wagorowa na Waburugi. Shughuli zao kuu za kiuchumi zilikuwa kilimo na ufugaji. Walilima mazao kama mahindi, mtama na uwele huku wakifuga ng’ombe, mbuzi, kondoo, punda na kuku. Utawala wao ulijengwa katika mfumo wa ukoo uliosimamiwa na baraza la wazee. Wazee walikuwa na jukumu la kusuluhisha migogoro, kusimamia sheria, kufanya matambiko ya kidini na kutoa maamuzi muhimu kuhusu jamii. Katika familia, baba alikuwa mkuu wa kaya. Jamii hizi ziliamini kuwepo kwa mizimu na zilizingatia mila na desturi mbalimbali. Elimu ya jando na unyago ilitumika kuwafundisha vijana haki, wajibu na maadili ya jamii. Vijana walifundishwa kufanya kazi kwa bidii, kuwa jasiri na kujitegemea. Pia ndoa za wake wengi zilikuwa sehemu ya utamaduni wao, na urithi mara nyingi ulitolewa kwa watoto wa kiume. Sherehe mbalimbali za kitamaduni zilifanyika kulingana na matukio na majira ya mwaka. Jamii za Wanilo Wanilo ni jamii inayojulikana zaidi kwa shughuli za ufugaji. Walifuga ng’ombe, mbuzi, kondoo na punda. Punda walitumika kubeba mizigo wakati wa kuhama kutafuta malisho na maji. Mifano ya jamii za Wanilo nchini Tanzania ni Wamasai, Wajaluo na Wadatoga. Mfumo wao wa kisiasa ulijulikana kama utawala wa kirika. Mfumo huu uliwagawa watu kulingana na umri na majukumu yao katika jamii. Vijana wa Kimasai wanaojulikana kama Morani walikuwa walinzi wa jamii na mifugo. Walikuwa na jukumu la kulinda ardhi, kutafuta malisho na maji pamoja na kupambana na maadui. Wanawake walijishughulisha na kazi za nyumbani kama kujenga nyumba, kuandaa chakula, kutafuta kuni na kulea watoto. Watoto walisaidia kuchunga ndama na mifugo midogo. Wazee walikuwa kundi lenye mamlaka makubwa zaidi katika jamii. Walitoa maamuzi muhimu, kutatua migogoro na kusimamia masuala ya kijamii. Kiongozi mkuu wa kisiasa katika jamii ya Kimasai aliitwa Ol-aiguanani, ambaye alikuwa na mamlaka makubwa juu ya jamii nzima. Umuhimu wa Jamii za Asili kwa Tanzania Jamii za asili za Tanzania zimechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya taifa. Zimetufundisha maadili ya ushirikiano, uwajibikaji, uaminifu, kuheshimu wazee, kufanya kazi kwa bidii na kuishi kwa amani. Pia zimechangia maendeleo ya kilimo, ufugaji, biashara, uvuvi, utawala na utunzaji wa mazingira. Hadi leo, baadhi ya mila, desturi na mifumo ya uongozi wa jamii hizi bado inaendelea kutumika katika maisha ya Watanzania.

    KAZI YAKUFANYA

    1. Taja shughuli kuu za kiuchumi zilizofanywa na jamii za Kibantu.
    2. Kwa nini jamii za Kibantu ziliweza kufanya kilimo kwa mafanikio makubwa?
    3. Eleza majukumu manne ya kiongozi wa ukoo katika jamii za Kibantu.
    4. Jando na unyago vilikuwa na umuhimu gani katika jamii za Kibantu?
    5. Taja makabila matatu yanayounda jamii za asili za Zanzibar.
    6. Eleza shughuli kuu za kiuchumi zilizofanywa na jamii za Wakichembe.
    7. Ni maadili gani muhimu yaliyofuatwa na jamii za Wakichembe katika matumizi ya rasilimali za mazingira?
    8. Fafanua mfumo wa utawala uliotumiwa na jamii za Wakushito.
    9. Morani katika jamii ya Kimasai walikuwa na majukumu gani?
    10. Eleza mchango wa jamii za asili za Tanzania katika kukuza maadili ya ushirikiano, uaminifu na amani.
    11. Kuna faida gani za kujifunza historia ya jamii za asili za Tanzania?
    12. Je, ni maadili yapi kutoka jamii za kale ambayo yanaweza kusaidia kutatua changamoto za jamii ya leo?
    13. Linganisha shughuli za kiuchumi za Wakichembe, Wakushito na Wanilo.
    14. Kwa nini wazee walikuwa na nafasi muhimu katika mifumo ya utawala wa jamii za asili?
    15. Eleza jinsi biashara ilivyochangia maendeleo ya jamii za Zanzibar.

    Maadili ya Jamii za Asili za Kitanzania

    Kwa kiasi kikubwa, maadili ya jamii yoyote hujengwa na kuongozwa na mila na desturi za jamii husika. Maadili haya yanaweza kutofautiana kutoka jamii moja kwenda nyingine kulingana na mazingira, shughuli za kiuchumi, utawala na utamaduni wa watu wanaohusika. Ndani ya jamii moja pia kunaweza kuwapo makundi mbalimbali yenye maadili maalumu yanayowaongoza katika maisha yao ya kila siku. Hivyo, maadili yanaweza kuwa ya jamii nzima au ya kundi fulani ndani ya jamii. Maadili yana nafasi muhimu katika maisha ya binadamu kwa sababu huwasaidia wanajamii kuishi kwa kufuata kanuni na mwenendo unaokubalika. Kupitia maadili, migogoro hupungua na jamii huweza kuishi kwa amani, upendo, mshikamano na ushirikiano. Aidha, maadili hujenga heshima, uwajibikaji na umoja miongoni mwa wanajamii. Jamii za Wabantu, Wakushito, Wakichembe na Wanilo zilikuwa na mila na desturi zilizolenga kujenga na kuimarisha maadili katika nyanja mbalimbali za maisha. Ingawa mila na desturi hizo zilikuwa tofauti kutokana na mazingira na mifumo yao ya maisha, kwa ujumla zilikuwa na malengo yanayofanana. Malengo hayo yalijumuisha: Kukuza na kuhimiza tabia njema katika jamii. Kuhamasisha watu kufanya kazi kwa bidii. Kuhimiza usawa katika uzalishaji, mgawanyo na matumizi ya rasilimali. Kukuza heshima na kuthamini utu wa kila mtu. Kuhakikisha malezi bora ya watoto na vijana. Kukuza ushirikiano na mshikamano miongoni mwa wanajamii. Kwa ujumla, mila na desturi za jamii hizi zililenga kuendeleza maadili katika nyanja za uchumi, elimu, imani, tabia, malezi na taratibu za maisha zilizokubalika katika jamii. Tabia Njema Mafunzo ya maadili katika jamii za asili yalisisitiza kujenga tabia njema kwa wanajamii wote. Mambo yaliyosisitizwa ni pamoja na: Kuwatunza wazee, watoto na watu wasiojiweza. Kuwajibika na kufanya kazi kwa bidii. Kuwa na ukakamavu, uhodari na ujasiri katika maisha. Kuwaheshimu wazee na watu wenye umri mkubwa kwa kuwa walionekana kuwa na hekima na uzoefu zaidi. Kushirikiana katika nyakati za furaha na huzuni kama vile harusi, misiba na sherehe mbalimbali. Kupenda na kuwakaribisha wageni kwa ukarimu. Kujenga mahusiano mazuri na kuepuka migogoro isiyo ya lazima katika jamii. Tabia hizi zilisaidia kudumisha amani, umoja na mshikamano katika jamii za asili za Tanzania. Elimu na Maarifa Mila na desturi zilikuwa njia muhimu ya kutoa elimu na maarifa kwa wanajamii. Elimu ilitolewa hasa kwa njia ya vitendo ndani ya familia na jamii kwa ujumla. Watu wazima, wazee na wenye uzoefu walikuwa na jukumu la kuwafundisha watoto na vijana stadi mbalimbali za maisha. Kwa mfano, katika jamii za Wakichembe vijana walijifunza uwindaji kwa kuandamana na watu wazima wakati wa mawindo. Pia walifundishwa matumizi ya dawa za asili kwa kuangalia jinsi wazazi wao walivyotumia mimea mbalimbali kutibu magonjwa. Vilevile, vijana walifundishwa maarifa kuhusu vita, uwindaji, tiba za asili, uhunzi, ufinyanzi, historia ya jamii, mila, desturi na imani za jadi. Elimu hiyo ililenga: Kujikinga na kutibu magonjwa ya binadamu na mifugo. Kukuza ushirikiano, upendo na udugu. Kuheshimu utu wa watu na kufuata utaratibu. Kujilinda dhidi ya majanga mbalimbali. Kuhifadhi na kuendeleza mila na desturi za jamii. Kupitia elimu hii, jamii ziliweza kuendeleza maarifa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine. Malezi na Makuzi Malezi katika jamii za asili yalitolewa kwa kuzingatia mila, desturi na maadili ya jamii husika. Malezi yalianza tangu mtoto akiwa tumboni mwa mama hadi alipofikia utu uzima. Wazazi na jamii walikuwa na jukumu la kuhakikisha mtoto anakua katika mazingira yanayomjenga kuwa mwanajamii mwema. Mama mjamzito alielekezwa kuhusu vyakula na tabia zinazofaa ili kupata mtoto mwenye afya njema. Baada ya kuzaliwa, mtoto alifundishwa maadili, heshima, nidhamu na wajibu wake katika jamii. Katika jamii za Wabantu kama Wazaramo na Wamakonde, vijana walipitia jando baada ya kufikia balehe. Wakiwa jandoni walifundishwa maadili mema, wajibu wa kifamilia, uongozi na namna ya kuwa baba bora. Wasichana walipitia unyago ambapo walifundishwa kuhusu maisha ya ndoa, malezi ya watoto na usimamizi wa familia. Familia na koo zilikuwa msingi wa malezi. Hata hivyo, jamii nzima ilikuwa na wajibu wa kushiriki katika malezi na makuzi ya watoto ili kuhakikisha wanakuwa watu wenye maadili mema na wanaokubalika katika jamii. Imani na Dini Imani na dini katika jamii za kale zilijengwa katika misingi ya mila na desturi za jamii husika. Jamii nyingi ziliamini uwepo wa Mungu kama muumba na mtawala wa vitu vyote. Pia waliamini uwepo wa mizimu ya mababu ambao walihusishwa na ustawi wa jamii. Kutokana na imani hizo, watu walimhusisha Mungu na vitu vikubwa vya asili kama jua, milima, mito, maziwa na misitu mikubwa. Waliamini kuwa Mungu ndiye mwenye mamlaka juu ya maisha ya viumbe vyote na matukio mbalimbali ya dunia kama mvua, ukame na mavuno. Jamii zilikuwa na taratibu maalumu za ibada zilizoitwa matambiko. Matambiko yalifanyika katika maeneo kama misitu, mapango, makaburi, milimani, kwenye miti mikubwa, mawe makubwa, ziwani au baharini kulingana na mila za jamii husika. Madhumuni ya matambiko yalikuwa kuomba mvua, mavuno mazuri, baraka, afya njema na kuondoa mikosi au majanga. Watu walitoa sadaka kama nafaka, wanyama na vinywaji vya jadi kama sehemu ya ibada. Matambiko haya yaliongozwa na wazee wa koo, waganga wa jadi au viongozi wa kimila. Aidha, maeneo mengi yaliyotumika kwa matambiko yalilindwa dhidi ya uharibifu. Misitu na miti mikubwa iliheshimiwa na kutunzwa kwa sababu iliaminika kuwa sehemu takatifu. Hali hii ilisaidia kuhifadhi mazingira na rasilimali za asili. Katika jamii hizi pia kulikuwa na matumizi ya dawa za asili kwa ajili ya kutibu na kuzuia magonjwa. Waganga wa jadi, wakunga na wazee wa kimila walitumia mitishamba pamoja na maarifa ya jadi kutoa huduma za afya kwa wanajamii. Kwa ujumla, maadili yaliyotokana na imani na dini yalichangia kuimarisha nidhamu, umoja, heshima, uwajibikaji na kuhifadhi mazingira katika jamii za asili za Tanzania.

    KAZI YAKUFANYA

    1. Maadili ni nini na yana umuhimu gani katika jamii?
    2. Taja malengo manne ya ujenzi wa maadili katika jamii za asili za Kitanzania.
    3. Eleza namna mila na desturi zilivyosaidia kukuza tabia njema katika jamii.
    4. Bainisha tabia tano zilizosisitizwa katika jamii za asili za Tanzania.
    5. Elimu ya jadi ilitolewaje katika jamii za asili za Kitanzania?
    6. Taja malengo matatu ya elimu iliyotolewa katika jamii za asili.
    7. Fafanua nafasi ya familia na jamii katika malezi na makuzi ya watoto.
    8. Eleza umuhimu wa jando na unyago katika jamii za asili za Kitanzania.
    9. Matambiko yalikuwa na madhumuni gani katika jamii za kale za Tanzania?
    10. Ni kwa namna gani imani na dini za jadi zilichangia kuhifadhi mazingira na maadili katika jamii?
    11. Fafanua sifa inayotokana na jamii za asili za Wakushito. 
    12. Eleza jinsi maadili kuhusu imani na dini yalivyokuwa yakirithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine katika jamii za asili za Tanzania. 
    13. Eleza sababu zilizomfanya binadamu kuishi pamoja. 
    14. Kwa nini ni muhimu kufahamu historia ya jamii za asili za Kitanzania? 
    15. Toa mifano ya tabia za kuheshimu na kujali utu wa mtu mwingine kutoka katika jamii za asili. 
    16. Fafanua malengo ya ujenzi wa maadili katika jamii za asili za Kitanzania. 
    17. Eleza tofauti iliyopo kati ya maadili yaliyojengwa katika jamii za asili na jamii za sasa za Kitanzania. 
    18. Ni maadili gani ya jamii za asili yanayopaswa kuendelezwa ili kukuza na kujenga maadili katika jamii za sasa za Kitanzania? 
    19. Nini mchango wa maadili katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika jamii za sasa za Kitanzania? 
    20. Bainisha changamoto za kukuza maadili katika jamii unamoishi na kisha toa mapendekezo ya jinsi ya kuzitatua.

No comments:

Post a Comment