FORM ONE: HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI : DHANA YA MAADILI

 Maadili ni miongozo inayotawala tabia na matendo ya mtu mmojammoja au jamii kwa ujumla. Ni miongozo au maelekezo ya mienendo na matendo mema au kuwa na tabia njema. Katika muktadha huu neno maadili pia huashiria jitihada za kujua vigezo vya matendo yanayofaa na yasiyofaa katika jamii inayohusika. Neno maadili linapotumika huweza pia kuashiria au kumaanisha tunu za jamii au taifa. Kwa mfano, uhuru na amani ni tunu za taifa letu na mtu au kikundi cha watu kinapovunja amani au kubana uhuru na haki za binadamu, huwa tunasema wamevunja maadili au hawana maadili. 

Vilevile, maadili hujumuisha ushirikiano na mshikamano. Ushirikiano na mshikamano ni nyenzo muhimu katika jamii za Kitanzania kwani huimarisha jamii na kuboresha maisha ya watu. Ushirikiano na mshikamano hujidhihirisha kupitia kusaidiana katika kazi mbalimbali, matukio ya kijamii, na kusaidia majirani wakati wa matatizo. Aidha, jamii za Kitanzania ni maarufu kwa ukarimu kwa wageni. Wageni hukaribishwa kwa furaha na kupewa heshima kubwa ikiwa pamoja na kukirimiwa kwa chakula na malazi. Hivyo, ukarimu ni sehemu muhimu ya maadili ya Kitanzania. Umuhimu wa maadili kwa taifa unaweza kutazamwa katika mambo yafuatayo: 
(a)Kutambulisha utu wetu;
(b) Kukuza na kuendeleza uhusiano wa karibu miongoni mwa watu; 
(c) Kujenga heshima na uaminifu miongoni mwa watu; 
(d) Kujenga uhusiano miongoni mwa watu na mazingira yao; 
(e) Kuleta maendeleo; 
(f) Kujenga amani; 
(g) Kupunguza uhalifu na kuimarisha utii wa sheria; na 
(h) Upatikanaji wa haki, usalama na furaha katika jamii.

Kazi ya kufanya 1.2

Soma matini kutoka vyanzo mbalimbali ikiwamo maktaba mtandao na andika umuhimu mwingine wa historia ya Tanzania na maadili.

Zoezi la 1.2 

1. Ungepewa nafasi ya kuongoza klabu ya kusimamia maadili shuleni, ni mambo gani ungependa yajadiliwe kuhusu maadili? 
2. Unadhani ni vitu gani vinachangia kujenga tabia njema? 
3. Eleza uhusiano uliopo kati ya historia na maadili. 
4. Una ushauri gani kuhusu ujenzi wa maadili kwa watoto na vijana? 
5. Bainisha matendo ya kimaadili unayotenda au kutendewa na wenzako shuleni?

Kwa muktadha huu, dhana za historia na maadili zimetawala katika somo hili zikitambulisha matukio yaliyopita ya kijamii, kisiasa, na kiuchumi; miongozo, taratibu na kanuni zilizotawala tabia na matendo ya jamii za Kitanzania. 

Pia, dhana hizi zitawezesha kutambua kutoka katika historia ya taifa letu, maelekezo na fikra za kutuwezesha kutenda matendo mema au kuwa na tabia nzuri. Kwa maneno mengine, dhana za historia na maadili zinaelekeza kutambua vigezo vya matendo mema na mabaya katika jamii za Kitanzania za zamani na sasa, hivyo kuwezesha kujifunza au kujua maadili ya jamii ya Kitanzania za kale na za sasa.

KAZI YAKUFANYA

  1. Kwa nini jamii isiyo na maadili mazuri inaweza kushindwa kupata maendeleo hata ikiwa ina rasilimali nyingi?

  2. Je, amani na uhuru vinawezaje kuonyesha kuwa watu wa taifa fulani wana maadili mema? Toa mifano.

  3. Ungefanya nini ikiwa ungeona rafiki yako anafanya jambo linalokiuka maadili ya shule? Eleza sababu za uamuzi wako.

  4. Kwa nini ushirikiano na mshikamano vinachukuliwa kuwa sehemu muhimu ya maadili ya Kitanzania?

  5. Fikiria jamii ambayo watu wake hawana uaminifu. Ni matatizo gani yanaweza kutokea katika jamii hiyo?

  6. Je, ukarimu kwa wageni unaweza kusaidia kujenga sifa nzuri ya taifa? Eleza kwa hoja.

  7. Ni kwa namna gani kujifunza historia ya Tanzania kunaweza kusaidia vijana wa leo kuwa na tabia njema?

  8. Ikiwa watoto na vijana hawatafundishwa maadili tangu wakiwa wadogo, unadhani maisha yao na ya jamii yatakuwaje baadaye?

  9. Kati ya umuhimu wa maadili uliotajwa (amani, maendeleo, haki, usalama, uaminifu n.k.), ni upi unaouona kuwa muhimu zaidi? Toa sababu za jibu lako.

  10. Unadhani mtu mmoja mwenye maadili mema anaweza kubadilisha jamii nzima? Eleza kwa mifano au hoja zinazounga mkono jibu lako.

11. Andika insha fupi ya maneno 100–150 ukieleza jinsi maadili mema yanavyoweza kuifanya Tanzania kuwa taifa lenye amani, maendeleo na mshikamano.

No comments:

Post a Comment