FORM ONE: HISTORIA YA TANZANIA NA MAADILI

 

Utangulizi 

Ni muhimu kuenzi, kudumisha na kuhifadhi historia ya Tanzania na maadili kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo. Katika sehemu hii, utajifunza maana ya historia ya Tanzania, maadili na uhusiano kati ya somo Historia ya Tanzania na Maadili na masomo mengine. Umahiri utakaoujenga utakuwezesha kuthamini historia ya Tanzania, maadili na uzalendo na kueleza uhusiano kati ya somo la Historia ya Tanzania na Maadili na masomo mengine. 

Fikiri kuhusu somo la Historia ya Tanzania na Maadili.
Taja umuhumu wa somo hili?

Historia ya Tanzania na maadili 

Somo la Historia ya Tanzania na Maadili linaundwa na dhana kuu mbili. Dhana ya kwanza ni historia ya Tanzania na dhana ya pili ni maadili. Historia huhusu mambo au matukio yaliyopita yenye athari kubwa kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni katika jamii. Baadhi ya matukio hayo ni biashara ya watumwa, ukoloni na vita. Kwa mfano, ukoloni, si tu uliathiri utamaduni wa jamii pia ulileta utamaduni mpya katika jamii za Kitanzania. Kwa hiyo, historia ya Tanzania ni mfululizo wa matukio yaliyotokea nchini Tanzania yanayohusisha masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Historia hii inakumbusha mambo yaliyotokea katika jamii za Tanzania kwa lengo la kusaidia kuelewa tulikotoka, tulipo na kutafakari juu ya tunakokwenda. Historia ya Tanzania inazingatia mambo mbalimbali ambayo ni pamoja na: 
(a) Makabila mbalimbali katika nchi hii yalivyoendeleza utamaduni wao na jinsi mwingiliano kati ya makabila ulivyojenga utamaduni wa kitaifa; 
(b) Mabadiliko ya kijamii, kisiasa na kiuchumi katika jamii za Kitanzania, kama vile ya familia, elimu, na shughuli mbalimbali za kiuchumi katika jamii za Kitanzania; 
(c) Umuhimu wa kujenga utambulisho na mshikamano wa kitaifa kwa kuondoa tofauti za kikabila na kidini; 
(d) Utambuzi wa umuhimu wa kuwa na umoja na ushirikiano kama taifa;
(e) Maendeleo ya kiuchumi kutokana na kilimo na biashara za kijadi hadi uchumi wa kisasa; 
(f) Ukuaji na mabadiliko ya uchumi wa nchi katika vipindi mbalimbali na jinsi maendeleo hayo yalivyoathiri maisha ya jamii za Kitanzania; na 
(g) Kudumisha utamaduni, amani na ushirikiano kati ya makabila na dini mbalimbali. 

Kazi ya kufanya 1.1 

Soma matini kutoka vyanzo mbalimbali vya taarifa ikiwamo maktaba mtandao na bainisha mambo yanayoweza kufundishwa katika somo la Historia ya Tanzania na Maadili.

Zoezi la 1.1

1. Fafanua matukio mbalimbali ya kihistoria unayoyafahamu kuhusu Tanzania. 
2. Kwa nini ni muhimu kujua historia yetu? 
3. Eleza ni kwa namna gani historia ya Tanzania ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi. 
4. Kwa nini kujifunza na kuelewa historia ya Tanzania na maadili kunawezesha kujenga uzalendo? 
5. Kwa jinsi gani historia ya Tanzania na maadili inachangia katika kujenga utambulisho wa kitaifa?

No comments:

Post a Comment